Kairuki aahidi kujenga barabara tisa Goba

DAR-ES-SALAAM : MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kibamba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Angellah Kairuki, amesema endapo atapewa ridhaa ya kuongoza jimbo hilo, atahakikisha barabara tisa zilizopo katika Kata ya Goba zinajengwa ndani ya miaka mitano ya uongozi wake.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Goba, jijini Dar es Salaam, Kairuki alitaja barabara zitakazojengwa kuwa ni Goba Mjengo, Mtipesa, Kwa Makonda, Kwa Mwaipopo, TAG Matosa, Kwa Awadhi, Maendeleo Sheraton, Country Bus na Tatendo.
Kairuki alisema ujenzi wa barabara hizo utarahisisha usafiri wa wananchi na kuinua shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo. Amesema miongoni mwa vipaumbele vyake ni kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Goba, kgwa kujena uzio na kununua gari la polisi, ili kuongeza ufanisi wa kiusalama katika eneo hilo.
SOMA: Kairuki aahidi usimamizi huduma za kijamii
“Ninajua changamoto ya mgogoro wa ardhi katika eneo la DDC. Wapo wananchi waliotaabika kupata hati miliki, nitafanyia kazi suala hilo ili kupata suluhu ya kudumu,” alisema Kairuki. Ameongeza kuwa pia atahakikisha ujenzi wa daraja la Shule ya Sekondari Goba unaanza mapema, sambamba na kuongeza madarasa ya kidato cha tano na sita.
Kwa upande wa Mtaa wa Muungano, Kairuki alisema anafahamu hitaji la shule ya msingi katika eneo hilo na atahakikisha watoto hawavuki mto kwenda shule. Alibainisha kuwa atajenga kivuko cha lami kitakachounganisha Mtaa wa Muungano na Mivumoni.
Aidha, alisema shule ya sekondari katika mtaa huo ambayo imekamilika kwa asilimia 90, itaanza kutoa huduma mara baada ya uchaguzi. Kuhusu Mtaa wa Kunguru, Kairuki alisema atajenga barabara za ndani na kushughulikia changamoto za kijamii, ikiwemo mtoto aliyeachwa na baba yake ili apate huduma stahiki. Ameeleza kuwa kwa Mtaa wa Kisuku, atatekeleza ujenzi wa soko, barabara za ndani, na madaraja, yakiwemo Daraja la Kwa Baba Deni na Daraja la Kwa Silayo, ili kurahisisha usafiri na shughuli za wananchi.
Kairuki aliongeza kuwa kwa shule za Goba, atahakikisha ujenzi wa uzio na ukarabati wa miundombinu unakamilika, huku Zahanati ya Goba ikipandishwa hadhi kuwa Kituo cha Afya kitakachotoa huduma saa 24. “Tutashirikiana na mitaa na halmashauri kupata maeneo ya maziko ili kukabiliana na changamoto ya maeneo ya kuzikia,” alisema.
Aidha, aliahidi kutatua changamoto ya barabara inayounganisha Njia Nne – Matosa – Temboni, pamoja na vivuko na shule katika eneo la Kulangwa. Kairuki alisema kuwa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia ,Suluhu Hassan, maendeleo yataendelea kupelekwa Kibamba, ikiwemo kukamilisha hospitali, kuboresha huduma za afya na kuongeza vifaa tiba.
Kuhusu sekta ya elimu, alisema atahakikisha shule zinakarabatiwa kuwa za kisasa, kuongeza madawati na kuboresha shule ya mahitaji maalumu iliyopo katika eneo hilo. Kwa upande wa maji, Kairuki alisema licha ya huduma kupatikana kwa kiwango kikubwa, atahakikisha hakuna wananchi wanaotozwa bili za kubambikizwa, na kwamba ataweka mfumo wa mita za Luku za maji ili kudhibiti upotevu wa mapato.
Aliongeza kuwa kupitia halmashauri, serikali itaendelea kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, sambamba na mafunzo ya biashara. “Tutaleta fursa za ajira kwa vijana na bodaboda, tutasaidia kupata mikopo ili waweze kununua vyombo vyao vya usafiri. Akinamama nao watanufaika kupitia mikopo ya serikali,” alisema Kairuki.
Amesema pia atasimamia urasimishaji wa ardhi, ujenzi wa masoko, upatikanaji wa daladala za uhakika, na kuhakikisha watu wenye ulemavu na vijana wananufaika na fursa za kiuchumi zilizopo jimboni humo.



