Kairuki aahidi kutatua migogoro ya ardhi Msigani

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kibamba, Angellah Kairuki, ameainisha vipaumbele 10 atakavyotekeleza katika kata ya Msigani ikiwa atachaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.

Akizungumza katika kampeni zake, Kairuki alisema kuwa vipaumbele vyake ni kutatua migogoro ya ardhi inayoendelea, urasimishaji wa ardhi, kujenga zahanati, shule za msingi na sekondari, vituo vya polisi, soko la kudumu, ukarabati wa barabara za mitaani, na kuchukua hatua za kudumu kudhibiti mmomonyoko wa kingo za Mto Mbezi.

“Nitahakikisha ninatoa fursa za ajira kwa vijana, ajira rasmi na zisizo rasmi katika sekta binafsi, tutawaunganisha na fursa zingine. Pia tutaendelea na mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu bila kuwasahau wazee wetu. Nitapambana pia kutetea haki za kisheria za wajane kupata fursa za kiuchumi,” alisema Kairuki. SOMA: Serikali bega kwa bega na wafugaji Ngorongoro

Aidha, Kairuki alibainisha kuwa watahakikisha walemavu wanapata mitaji ya biashara, huduma za kijamii, na shule zenye mahitaji maalum katika kata ya Kibamba. Alisisitiza kuwa CCM ina maneno machache lakini vitendo vingi vinavyoonekana, na kuwaomba wananchi kumpigia kura ili kuendeleza miradi ya maendeleo.

Kairuki pia alieleza mafanikio yaliyofanikishwa tayari katika kata hiyo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule za msingi zikiwemo Bwawani, Malamba Mawili, Msigani, Msingwa na Temboni, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa madawati ya kutosha na matundu ya vyoo kwa wanafunzi na walimu.

Mbali na hapo, wamejenga zahanati ya Msingwa yenye gharama ya Sh 211 milioni, na zahanati ya Temboni yenye gharama ya Sh 100.99 milioni, pamoja na kuweka hema la kupumzikia. Pia, wananchi wameweza kufaidika na mikopo ya Sh 616.6 milioni kwa vikundi vya nyumbani, wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Kairuki alisema kuwa karabati ya barabara za ndani imegharimu Sh 10.4 bilioni. Kata ya Msigani ina kilomita 5.3 za barabara zenye lami na zege, huku kilomita 38.4 zilizobaki zikiwa katika kiwango cha udongo na changarawe, ambazo pia zitawekwa hadhi ya lami na madaraja ya kutosha.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button