Kairuki aahidi usimamizi huduma za kijamii

DAR ES SALAAM: MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kibamba kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Angellah Kairuki amesema endapo wananchi wa kata ya Saranga watamchagua atahakikisha miundombinu ya barabara,maji, zahanati na shule zinakamilika kwa muda mfupi.
Akizungumzia wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu zilizofanyika katika Kata ya Saranga iliyopo katika Jimbo la Kibamba jijini Dar es Salaam, Kairuki pia amesema serikali itaendelea kuwawezesha wafanyabiashara wa bodaboda, bajaji na wamachinga kufanya biashara katika mazingira salama, huku akiahidi kufuatilia upatikanaji wa vyoo katika maeneo ya biashara yasiyo rasmi ili kuepusha milipuko ya magonjwa.
“Nikipata ridhaa nitasimamia ujenzi wa shule mpya katika mtaa wa Upendo ili kuondoa adha ya watoto kutembea umbali mrefu kufuata elimu, nitafuatilia utekelezaji wa miradi sita ya barabara, ikiwemo Kimombo, Taabu, Suka, Ukombozi na Peponi–KKT Temboni.
Ameongeza “Nitajitahidi kushughulikia changamoto ya ukosefu wa shule ya msingi katika mtaa wa Upendo, ambako watoto wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata elimu na wakati mwingine hupata ajali,nitafuatilia ujenzi wa shule mpya katika maeneo ya Kimarabaruti, King’ongo, Mavurunza na Salaga, pamoja na kuongeza madarasa na madawati katika shule zilizopo,”amesisitiza.

Kairuki amebainisha kuwa endapo atachaguliwa kuwa Mbunge wa Kibamba, ataendelea kusimamia miradi ya afya, elimu, maji, barabara na uwezeshaji wananchi kiuchumi, sambamba na kuhakikisha miradi ya maji ya Bangu, Pasaka na Ruvu Chini inakamilika kwa wakati.
Akizungumzia kuhusu baadhi ya mafanikio yaliyopatikana chini ya serikali ya CCM, Kairuki amesema serikali imewekeza Sh milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje, ambalo linatarajiwa kuanza kutumika mwezi Novemba mwaka huu.
“Serikali imefanikiwa kujenga jengo la ghorofa mbili katika Kituo cha Afya cha Kimara kwa gharama ya Sh milioni 427, pamoja na kununua vifaa vya hospitali vyenye thamani ya Sh milioni 100,CCM imewekeza Sh milioni 35.8 kujenga madarasa mapya na kutoa huduma ya chakula cha mchana kwa wanafunzi.

Amesema zaidi ya Sh bilioni 1.3 zimetumika kujenga madarasa 50, matundu ya vyoo 35, pamoja na ujenzi wa shule za sekondari za Ukombozi, Kigongona na Kisaranda kwa gharama ya shilingi milioni 377.
Kuhusu barabara, amesema zaidi ya Sh bilioni 1.8 zimetumika kujenga barabara za Kimombo, Suka, Kibongo, Sadaka na Sura, zikiwa katika viwango mbalimbali vya ujenzi, pamoja na mifereji ya maji ya mvua na kubainisha kuwa ujenzi wa kilomita 1.23 za barabara ya Kibanda cha Mkaa na Temboni Polisi unaendelea.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (CCM)Mary Chatanda amewahimiza wanawake kupiga kura na kuwahamasisha waume zao kupiga kura ifikapo oktoba 29 na Kumchagu Sk Sama Suluhu Hassan.
“Sisi wanawake tunafanye juhudi kuhakikisha mwanamke mwenzetu anapata kura na Rais Samia amefanya kazi kubwa wanawake muwe mstari wa mbele kuhakikisha anapita muwakubushe waume zenu kupiga kura na muwasisitize mara kwa mara kwa mahaba,”amesisitiza.
Ameongeza “Niwaambie wanakibamba kwa wagombea hawa mmelamba kidume
Samia amefanya mambo makubwa chama cha Mapinduzi kikavutiwa nacho kutokana na utendaji mzuri wa miaka iliyopita
Naomba nimuombee kura Samia itakapofika Oktoba 29 na Kariuki lakini diwani msimsahau.
Mgombea Udiwani Kata ya Saranga kupitia Chama chaMapinduzi (CCM)John Sanga
amesema Serikali imewapa Sh milioni 60 kwaajili ya ukarabati wa vifaa kwenye upande wa maji, usambazaji wa mabomba unaendelea imejenga tenki la maji la Bangulo na Goba linatuhudumia wananchi.



