Kamati yaitaka ofisi ya CAG kukagua kituo cha afya Farkwa

DODOMA: KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeiagiza Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum katika mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Farkwa, kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, mkoani Dodoma baada ya kubainika kuwa miundombinu ya kituo hicho haionyeshi thamani halisi ya fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya mradi huo.
Mwenyekiti wa LAAC, Halima Mdee, ametoa maelekezo hayo baada ya kamati kufanya ziara ya kukagua miradi ya ujenzi, ikiwemo Shule ya Msingi Sankwaleto na Kituo cha Afya cha Farkwa katika Halmashauri ya Chemba.

“Kamati inaagiza CAG kufanya ukaguzi maalum kwenye kituo hiki cha afya cha Farkwa, kwa sababu Kamati imebaini kuwa hakuna thamani ya fedha hapa,” amesema Mwenyekiti Mdee.
Aidha, Kamati hiyo pia imeielekeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi inayoendeshwa katika Halmashauri ya Chemba ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na inaendana na thamani ya fedha iliyotolewa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dk. Festo Dugange, amesisitiza umuhimu wa usimamizi thabiti wa miradi ya maendeleo ili fedha zinazotolewa na serikali ziweze kuleta manufaa kwa wananchi.
“Serikali inaleta fedha kwa ajili ya kuhudumia wananchi, na kuna wataalamu wa kutosha kusimamia miradi hiyo. Sera ya serikali ni kusogeza huduma kwa wananchi, hivyo fedha ikitolewa, tuisimamie vizuri ili thamani yake ionekane kwenye miradi yetu,” amesema Dk. Dugange.



