Kambi Mbwana achukua fomu INEC Kwamatuku

PAZIA la uchukuaji fomu ya kugombea udiwani katika wilaya ya Handeni, imefunguliwa leo Agosti 18, 2025, huku mwandishi wa habari na mdau wa maendeleo Kambi Mbwana, akichukua fomu yake ya kuwania nafasi hiyo katika ofisi za Kata ya Kwamatuku, wilayani Handeni mkoani Tanga.
Tukio la uchukuaji fomu limeongozwa na viongozi wa Kata wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku wakisindikizwa na shamra shamra za wapenzi na wananchi wa Kata hiyo.
Akizungumza wakati wa kuchukua fomu yake, Mbwana amesema ameamua kuwania nafasi hiyo ili ashirikiane na wananchi katika kuendeleza na kusimamia sera na ilani ya chama chao, chini ya Mwenyekiti wao wa CCM Taifa, Dk Samia Suluhu Hassana ambaye pia ni mgombea urais wa Tanzania.
“Nakishukuru chama changu CCM kwa kuniamini na kunipa nafasi hii ambayo nimeitimiza kwa kuchukua fomu za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na kushuhudia shangwe za wananchi wenye mapenzi na mimi sambamba na uongozi wa Dk Samia ambaye kwa namna moja ama nyingine wameniamini.

“Baada ya kuchukua fomu, taratibu nyingine zitaendelea huku nikiwaomba wananchi wa Kata yetu na Watanzania wote wahakikishe Oktoba 29 wanajitokeza kupiga kura,” amesema.
Katika mchakato wa kura za maoni zilizofanyika Agosti 4, mwaka huu Mbwana aliibuka na ushindi kwa kupata kura 439.Mpinzani wake, Mustafa Beleko aliyekuwa anawania nafasi hiyo kwa kipindi cha nne, alipata kura 207 na mshindi wa tatu Joseph Minango amepata kura saba.
Vikao vya mwisho vya uteuzi katika ngazi ya mikoa kwa madiwani vilikamilika Agosti 13 mwaka huu tayari kwa wagombea hao kuwania nafasi hizo katika Uchaguzi Mkuu.



