Kampeni za uchaguzi ziwe za kistaarabu

USTAARABU katika kampeni ni jambo muhimu sana ili kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unaendeshwa kwa kuzingatia heshima, uwazi, usawa, kupinga chuki binafsi na matumizi ya kejeli katika kipindi chote cha kampeni za uchaguzi. Tunaweza kusema ustaarabu ni lugha ya heshima na sauti ya umoja, mazungumzo kwa lugha ya heshima yanaleta upendo na umoja hata kwenye maisha ya kawaida ya kila siku.

Kwa ujumla, ustaarabu katika kipindi cha kampeni unatengenezwa kwa ushirikiano wa pamoja wa vyama vya siasa, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, serikali na wananchi ambao ndio wapigakura, ili kuendeleza demokrasia imara, uchaguzi uwe huru na wa haki. Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, anaagiza vyama vya siasa vifanye kampeni za kistaarabu kwa kuzingatia sheria za nchi.

Nikinukuu maneno yake, Jaji Mutungi anasema: “Kuna msemo maarufu unasema kuna maisha baada ya uchaguzi, hivyo tusije tukadhani kuwa kila kitu kwetu ni uchaguzi pekee, amani na umoja wa taifa vipewe kipaumbele chake”. Naungana na Jaji Mutungi kuwakumbusha wagombea kuhakikisha wanafanya kampeni zao zote kwa msingi wa amani na utulivu, kuepuka maneno ya kashfa, matusi na chuki.

Wanatakiwa watambue kampeni ni nafasi ya kujadili ajenda si kuhamasisha mgawanyiko na chuki. Pia, wanatakiwa kuhakikisha wapigakura wao wanajua mipango yao kwa kunadi ilani yao kwa kueleza sera na jinsi watakavyotekeleza ahadi zao. SOMA: Kisesa wameitika mapokezi ya Nchimbi

Kampeni za kistaarabu zinahusisha uwazi kwenye mpango, dhamira, na matumizi ya rasilimali za nchi wakati mgombea atakapopewa ridhaa na wananchi. Nashauri kampeni zisiwe za propaganda za uchochezi badala yake ziwe zenye kuzingatia maadili, mijadala iwe ya kuzungumza mambo yenye uhalisia na si upotoshaji. Ahadi zilenge maendeleo ya jamii ikiwemo ubora wa elimu, huduma za afya, usalama wa umma na huduma nyingine za msingi.

Rais wa Kwanza wa Afrika Kusini na Baba wa taifa hilo, Nelson Mandela aliwahi kusema: “Uongozi bora ni ule unaopigania ustawi wa watu wote.” Kwa mfano wa kauli hii, wagombea wanatakiwa wazungumze na wapigakura wao kwa kuwaeleza mikakati yao katika kupigania ustawi wa jamii na si vinginevyo. Kwa kuzingatia dhana ya ‘kuna maisha baada ya uchaguzi’ kampeni zinapaswa kuendeshwa kwa misingi ya sheria, kanuni, miongozo, maadili na mtazamo chanya kwani baada ya kampeni kuna kupiga kura na kisha maisha baada ya uchaguzi kila mtu na eneo lake na kazi kuleta maendeleo na ustawi wa jamii.

Hivyo Watanzania tunapaswa kuelewa kampeni si ushindani mbaya wala vurugu bali ni jukwaa la kutoa maoni, kusikiliza sera, kupata uelewa, ubishani wa hoja na kufanya uamuzi wa nani umchague atakayekuletea maendeleo. Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vingine kadhaa vya upinzani vimeahidi kufanya kampeni za kistaarabu ambazo hazihitaji kejeli wala matusi, hivyo hatutarajii yeyote kupenyeza hila, ubinafsi na matusi katika kampeni. Tuchague njia ya amani, maendeleo na heshima kwa kufanya kampeni za kistaarabu ili kubaki na Tanzania ya amani, kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button