Kanuni upigaji kura bajeti ya serikali kuboreshwa

DODOMA; BUNGE leo limepitisha mapendekezo ya maboresho ya Kanuni za Kudumu za Bunge, ambapo miongoni mwa maboresho hayo ni kuweka katika kumbukumbu kura za wabunge wanaotumia neno abstain kupiga kura zao.
Mapema leo asubuhi, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni za Bunge, Mussa Azzan. aliwasilisha taarifa ya kamati hiyo kuhusu Marekebisho au mabadiliko katika Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Februari 2023.
“Mheshimiwa Spika, kanuni hazijatambua utaratibu wa kuweka kumbukumbu ya kura za Wabunge wanaotumia neno abstain kupiga kura zao.
“Kutokana na kutotambulika katika kanuni kwa kura hiyo, imekuwa ni changamoto katika uwekaji wa taarifa za zoezi la kupiga kura.
“Hivyo, inapendekezwa suala hili lisimamiwe katika Kanuni ili kurekodi kura hiyo ya abstain. Vilevile inapendekezwa kuitambua kura hiyo kwa maneno Sipigi Kura ambayo ni tafsiri ya neno hilo katika lugha ya Kiswahili,” amesema Makamu Mwenyekiti huyo, ambaye pia ni Naibu Spika.