“Katiba CCM yawapa wastaafu jukumu la ushauri”

Mtaalamu wa Uchumi, Utawala Bora na Siasa, Dk Netho Ndilito, amemjibu kwa hoja Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Mhashamu Damian Denis Dallu, akimweleza kuwa viongozi wakuu wastaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaposhiriki kutoa ushauri, wanatekeleza jukumu lililo ainishwa kikatiba.

Dk Ndilito amesema Katiba ya CCM ya mwaka 2022, hususan Ibara ya 123 ukurasa wa 143, imeweka wazi wajibu wa viongozi wastaafu kuunda Baraza la Ushauri linaloshirikisha marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wa Zanzibar na makamu wa mwenyekiti wastaafu wa chama.

“Utaratibu huu ulianza tangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na umeendelea hadi sasa,” alisema.

Amesema awali, viongozi wastaafu walihudhuria kama wajumbe waalikwa wa kudumu katika Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa, kabla ya kuanzishwa rasmi kwa Baraza la Ushauri wakati wa uongozi wa Rais Jakaya Kikwete.

Kwa mujibu wa Ndilito, Baraza la Ushauri ndilo jukwaa rasmi la marais na viongozi wakuu wastaafu kushiriki kutoa mawazo na busara zao, na hivyo hakuna jambo la ajabu au lisilo na msingi katika ushiriki wao.

“Ni dhana iliyojengwa juu ya heshima, uadilifu na historia ya chama, na imepewa uhalali wa kikatiba,” amesema.

Kwa maana hiyo amesema, viongozi hao wanaposhiriki katika masuala ya chama, wanatekeleza wajibu waliopewa kwa mujibu wa Katiba ya CCM.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button