Ruto: Masoko ya China ni muhimu

NAIROBI, KENYA: RAIS wa Kenya, Dk. William Ruto, amesema kuwa uamuzi wa Kenya katika sera za mambo ya nje unaongozwa kwa maslahi ya taifa , huku akijibu hatua ya Marekani ya kutaka kupitia upya hadhi ya Kenya kama mshirika mkuu asiye mwanachama wa NATO.
Akizungumza na wawakilishi wa sekta binafsi nchini humo, Rais Ruto amesema kuwa serikali yake inalenga kuhakikisha kuwa sera za biashara na uhusiano wa kimataifa zinawanufaisha Wakenya, hasa wazalishaji wa ndani na wakulima.
“Baadhi ya marafiki zetu wanalalamika kuwa tunafanya biashara kubwa na China. Nilipokutana na Rais Xi Jinping, nilimweleza kuwa tunaagiza bidhaa za Shilingi bilioni 600 kutoka China, lakini mauzo yetu kwao ni asilimia tano tu. Hii sio sawa,” alisema Rais Ruto.
Alieleza kuwa China imekubali kufungua soko lake kwa bidhaa za kilimo kutoka Kenya ikiwemo chai, kahawa, parachichi na mazao mengine, bila ushuru.
“Wamekubali kusaidia kurekebisha hali ya biashara kati ya Kenya na China kwa kuondoa ushuru kwenye bidhaa zetu za kilimo,” alisema Rais Ruto, huku akibainisha kuwa mazungumzo kama hayo yanaendelea pia na mataifa ya India, Uturuki na Canada. SOMA: Tanzania, Kenya zazindua mkongo wa mawasiliano
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ulinzi ya Kenya, Nelson Koech, amemwandikia barua Seneta wa Marekani Jim Risch, akimuomba kufikiria upya mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Uidhinishaji wa Kitaifa wa Ulinzi (NDAA) ya Marekani kwa mwaka 2026.
Katika barua hiyo, Koech ameonya kuwa iwapo mapendekezo hayo yatapitishwa, yataweza kujumuisha tathmini ya sera za kigeni za Kenya, ikiwemo ushirikiano wake na mataifa kama China, Urusi na Iran, pamoja na tathmini ya uhusiano wa kisiasa au kifedha na makundi yenye silaha kama al-Shabaab na Rapid Support Forces (RSF) ya Sudan.
Hadi sasa, hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na Serikali ya Marekani kuhusu iwapo hadhi ya Kenya kama mshirika mkuu asiye mwanachama wa NATO itabadilishwa, huku wachambuzi wa masuala ya diplomasia wakiendelea kufuatilia kwa karibu uhusiano kati ya nchi hizo mbili.