Kenya yashindwa kufadhili elimu

NAIROBI : SERIKALI ya Kenya imetangaza kushindwa kumudu gharama za kufadhili elimu ya bure kwa shule za msingi na sekondari, hatua itakayoathiri maelfu ya wanafunzi na kuongeza mzigo kwa wazazi.
Akizungumza Julai 24, 2025 mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa, Waziri wa Fedha John Mbadi amesema ufadhili wa masomo ya bure umekuwa mzigo mkubwa kwa serikali kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi shuleni, hali iliyosababisha kupunguzwa kwa bajeti ya sekta ya elimu. “Kiwango cha ufadhili kwa shule ya sekondari kitapunguzwa kutoka Sh22,244 hadi Sh16,900 kwa kila mwanafunzi”.
Aliongezea kuwa, “Kwa sasa, wanafunzi wa shule za msingi hupokea Sh1,420, shule za sekondari za chini Sh15,042 na shule za sekondari za juu Sh22,244 kwa kila mwanafunzi,” alisema Waziri Mbadi. SOMA: “Nasema Siondoki” William Ruto
Aidha amesema kutokana na changamoto za kifedha na vipaumbele vipya serikalini, ongezeko la viwango vya ufadhili kwa sasa haliwezekani, lakini linaweza kuzingatiwa iwapo mapato ya serikali yataimarika.
Waziri wa Elimu Julius Ogamba amesisitiza kuwa ongezeko la idadi ya wanafunzi limekuwa kubwa zaidi kulingana na bajeti iliyotengwa kwa wizara hiyo katika miaka minne hadi mitano iliyopita. “Idadi hii haijawahi kushuhudiwa katika bajeti ya elimu. Wanafunzi wanaongezeka, lakini fedha zilizotengwa hazijabadilika,” alisema Ogamba.
Ukosefu wa ufadhili wa serikali katika sekta ya elimu nchini humo utawalazimisha wazazi kuchangia zaidi ili kufanikisha upatikanaji wa elimu kwa watoto wao.



