Kenya yaokoa raia watatu Urusi

NAIROBI : SERIKALI ya Kenya imesema imefanikiwa kuwaokoa raia wake watatu waliokuwa wamesafirishwa nchini Urusi na kulazimishwa kujiunga na jeshi la nchi hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Korir Sing’oei, amesema kuwa wanaume wawili na mwanamke mmoja wako salama na tayari wanarejea nyumbani kuungana na familia zao. Hatua hiyo inakuja wiki moja baada ya wizara hiyo kuthibitisha kuwa inafuatilia ripoti za Wakenya kadhaa waliolazimishwa kuingia jeshini Urusi na baadaye kutekwa vitani nchini Ukraine.
Katika taarifa hiyo, Sing’oei alisema raia hao waliokolewa kwa msaada wa ubalozi wa Kenya mjini Moscow, baada ya serikali kufuatilia taarifa zilizohusisha mtandao wa usafirishaji haramu wa watu. Aidha, jumamosi iliyopita vyombo vya usalama nchini Kenya vilifanya operesheni jijini Nairobi na kubaini kundi linalodaiwa kuhusika na uhalifu huo, kwa kuwarubuni raia kwa ahadi za ajira zenye maslahi makubwa Urusi. SOMA: Putin: Msitumie Mali za Urusi
Hata hivyo, mara baada ya kufika Moscow, vijana hao walilazimishwa kuingia kwenye jeshi na kupelekwa mstari wa mbele wa vita dhidi ya Ukraine. Kesi hiyo imeendelea kuvutia hisia ndani na nje ya Kenya, hususan baada ya jeshi la Ukraine kutoa video ya mwanariadha Mkenya aliyesema alihadaiwa kujiunga na jeshi la Urusi na kuomba msaada wa kurejeshwa nyumbani.



