Kesi ya kupinga tozo za miamala yasikilizwa

KESI ya kupinga tozo za miamala ya fedha kwa njia ya simu iliyofunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), imesikilizwa jana kwa upande wa walalamikiwa ambao ni serikali kuwasilisha pingamizi la awali mbele ya Jaji John Mgeta.

Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata aliwasilisha pingamizi hilo kwa kujikita katika sababu tatu walizoziona ni za msingi.

Sababu ya kwanza, alidai maombi yaliyotolewa na walalamikaji hayakuwa na msingi kwani hakuna uamuzi wowote uliotolewa unaohitaji kufutwa na mahakama.

Alisema walichofanya walalamikiwa ni kutimiza wajibu wao wa kikatiba kutafuta chanzo cha mapato.

Aliendelea kudai kuwa maombi hayo pia hayana msingi kwa sababu yaliwasilishwa na taasisi bila kuwa na maamuzi ya bodi huku akifafanua kuwa taasisi inapotaka kufungua shauri, lazima kuwepo uamuzi unaotoka kwenye bodi.

Alidai katika malalamiko yaliyotolewa, hakuna ushahidi unaoonesha kwamba bodi iliidhinisha kufunguliwa kwa kesi na kuongeza kuwa, huyo Anna Henga alipaswa kufungua shauri hilo mwenyewe na siyo  kupitia LHRC.

Pia aliongeza kuwa, katika malalamiko yake mlalamikaji hakuonesha namna gani anavyoathiriwa na uamuzi huo wala hakuonesha maslahi yake.

Akijibu hoja hizo, Wakili Mpore Mpoki anayewakilisha upande wa walalamikaji, alidai sheria inaruhusu ikiwemo ile iliyoanzisha tozo kupingwa mahakamani kama ilivyofanyika.

Kuhusu uamuzi wa bodi, Wakili Mpore alidai siyo pingamizi la kisheria kwa sababu ni suala linalohitaji ushahidi kwa kuwa aliyeapa alionesha dalili kwa namna gani kaathirika kwa niaba ya umma na ana maslahi katika shauri hilo.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 8, 2021 kwa ajili ya kutolewa uamuzi.

Shauri hilo Namba 11 lilifunguliwa Julai 27, 2021 kuomba Mahakama Kuu kufanya mapitio katika sheria ya mfumo wa taifa wa malipo pamoja na kanuni zilizotumika kuweka tozo katika miamala ya fedha kwa njia ya simu ambalo LHRC waliliona kama mzigo kwa raia na wafanyabiashara wadogo.

Kesi hiyo ni matokeo ya kupitishwa kwa mapendekezo ya bajeti ya serikali ya mwaka 2020/2021 iliyoelekeza kuwekwa kwa tozo hizo zilizoibua mijadala miongoni mwa raia huku baadhi yao wakizitafsiri kama mzigo kwa wananchi wakati upande wa serikali kupitia Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba wakielezea kuwa tozo hizo zitaleta tija katika maendeleo ya nchi ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Katika bajeti kuu iliyopitishwa na Bunge Juni mwaka huu, serikali ilianzisha tozo ya Sh 10 hadi Sh 10,000 katika kila muamala wa kutuma na kutoa pesa jambo lililoibua mijadala.

Habari Zifananazo

Back to top button