Kigoma kuiunganisha Tanzania kimataifa

KIGOMA: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu-Kazi Maalum, George Mkuchika amesema kuwa serikali imedhamiria kutekeleza na kukamilisha miradi yote ya miundo mbinu mkoani Kigoma ili kuiunganisha Tanzania kimataifa.

Waziri Mkuchika amesema hayo Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma akianza ziara ya siku nne mkoani humo kutembelea miradi na kufanya mikutano ya hadhara na wananchi kueleza kazi kubwa inayofanywa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Kazi Maalum, George Mkuchika akitembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa uboreshaji na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma

Katika ziara hiyo Waziri Mkuchika ametembelea mradi wa maboresho na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma, kutembelea bandari ya Kigoma na kukagua utekelezaji wa miradi ya ukarabati wa meli za Mv.Liemba na MT Sangara na kusema kuwa miradi yote ambayo serikali inatekeleza itakamilishwa.

“haya yote yanayofanyika sasa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi, Rais Samia ametutuma mawaziri wake kutembelea na kukagua miradi na ambayo iko tayari tuizindue iendelee na kazi na hiyo inaonyesha kazi kubwa na iliyotukuka iliyofanywa na Rais wetu”, amesema Waziri Mkuchika.

Meneja wa TANROADS Mkoa Kigoma Narcis Choma (kushoto) akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa uboreshaji na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Kazi Maalum, George Mkuchika anayefanya ziara ya kiserikali ya siku nne mkoani Kigoma

Awali akitoa taarifa kwa Waziri Mkuchika Meneja wa Wakala wa barabara (TANROADS) Mkoa Kigoma, Narcis Choma alisema kuwa mradi wa uboreshaji wa uwanja wa ndege wa Kigoma utahusisha jengo la kuondokea na kufikia abiria, ujenzi wa uzio wa uwanja, mnara wa kuongozea ndege na taa katika barabara za kuongozea ndege.

Choma alisema kuwa mradi huo utagharimu kiasi cha Sh bilioni 46.6 chini ya Kampuni ya China Railways Engineering ukiwa mradi wa miezi 18 na kwamba kukamilika kwa mradi huo kutaongeza idadi ya abiria wanaotumia uwanja wa ndege wa Kigoma kufikia 400,000 kutoka chini ya 100,000 wanaosafiria kupitia uwanja huo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button