Kikwete: Mwinyi alikuwa mpole, mkali, alitufukuza

alinianzishia safari ya kuwa Rais

DAR ES SALAAM: RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ametoa simulizi ya Hayati Rais  Ally Hassan Mwinyi kuwa alikuwa ni mpole lakini pia alikuwa ni mkali na mwenye maamuzi magumu.

Akitoa simulizi ya Hayati Mwinyi, leo Machi Mosi, 2024  wakati akitoa salamu za pole kwa familia, Kikwete amesema alimfahamu Mzee Mwinyi wakati akiwa Waziri.

“Nilikuwa namsoma akiwa Waziri baadae akajiuzulu akawa balozi akarudi akawa waziri kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais, alikuwa ‘low profile’, hakua kimbelembele kuonekana sana,” anasimulia Kikwete na kuongeza

“Nilifamhamu sana mwaka 1984 wakati wa machafuko ya hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar, kulikua na mkutano wa halmashauri ya taifa (NEC) ulifanyika Dodoma na mimi nilikuwa mjumbe ndio nilikuwa nimeingia miaka miwili tu.

“Wajumbe wote tulipangiwa kulala kwenye hosteli za Chuo cha Biashara (CBE), si kawaida, maana tunapewa posho yetu tunaenda kulala unapojua, baadae tukaenda kusimuliwa kujua kwa nini ilikuwa vile.

“Lakini Mawaziri walikuwa wanalala majumbani kwao, tulikuwa na Waziri mmoja tu aliyekuja kukaa na sisi mwayangu mwayangu, Waziri huyo ni Ally Hassan Mwinyi tukafanya udadisi kwa nini? tukaja kujua ile ‘rest house’ chumba cha mapumziko alikopangiwa kukaa, Waziri mwenzake aliamua kumuweka mtu mwingine.

“Kwa hiyo alijua ndio chumba chake cha siku zote akakuta mgeni mwingine, akaamua kutokugombana na kuja kujiunga na sisi wajumbe wa kawaida wa NEC, alitupa mapenzi makubwa, hakuwa anadai ‘treatment’ tofauti na sisi.

“Tulijifunza ni mtu hapendi makuu, anaishi maisha ya kawaida kama watu wengine ana mapenzi kwa watu, mchakato ulivyokuwa unakwenda baada ya Mzee Jumbe (Aboud) kujiuzulu mzee Mwinyi akapendekezwa, mpendekezaji sheikh Thabiti Kombo sisi tuliokuwa tunakaa nae hosteli tulifurahi maana tulikuwa tumeshamfahamu na tukasema Zanzibar watakuwa wamepata kiongozi thaibiti.

“Pengine yule aliyemkataa kule Mwenyezi Mungu alimuongoza Mwinyi aje kukaa na sisi ili wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) tumfahamu, atufahamu.” amesema Kikwete

MAFUNZO MAKUU MATATU

“Chumba chake cha siku zote anachofikia kupewa mtu mwingine na kuondoka bila kugombana kwangu lilikuwa ni funzo kubwa, tusihamanike mambo yanapotokea uwenda kuna sababu yake Mwenyezi Mungu aliyefanya hayo yatokee.

Funzo la Pili: Kumfahamu Mzee Mwinyi ni pale aliponiteua kuwa Mbunge na Naibu Waziri wa Nishati na Madini mwaka 1988, nilikua jeshini nikateuliwa kuwa Katibu wa Chama wa wilaya ya Nachingwea baadae katibu wa CCM Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.

Katika simulizi hiyo, Kikwete anasema siku alivyomteua kuwa Mbunge na hapo hapo akamteua kuwa Naibu Waziri ndio aliona upande wa pili wa Mzee Mwinyi kuwa ni mkali..

Kikwete anasema alipokwenda ofisini kwake kumuona, wakati huo, Kikwete alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) CCM, vilevile Katibu wa CCM, Wilaya ya Masasi, Mtwara.

“Nilipokwenda kumuona nikamwambia hii ya ubunge ni nzuri, nitakuwa natoka Masasi mara nne kwenda vikao vya bunge lakini hili la Naibu Waziri silijui akaniambia ‘You are Young, Bright, Best of Luck’ akaniacha hakuwa na interest ya kuendelea kunisikiliza, na mie nikatoka nikarudi kwa katibu wa Rais Mahamoud Jabir….; “akaniambia mbona unaonekana umeloa sana ndio nikajitizama kumbe nilitokwa jasho sana kipindi kile nilichokuwa na Mzee, nikamwambia kukaa na Rais sio jambo dogo.

“Badae nikaja kuwa Waziri wa Maji Nishati na Madini, baadae nikawa Waziri wake wa Fedha, Rais Mwinyi alikuwa msikivu sana alikuwa anapokea ushauri, ukiwa mzuri.

Funzo la tatu: Kikwete anasema funzo lingine alilopata ni kuwa Mzee Mwinyi alikuwa ni mtu mwenye kuamua, alikuwa hana hulka kwenye kuamua, ukimuona unamuona kama mpole, rahimu, lakini jambo aliloliamini ili ni sawa na lina maslahi kwa taifa ataliamua…; “ni fundisho kubwa kwa viongozi, unaloliamini bora lina maslahi kwa taifa likomalie,

“Watanzania tumkumbuke ndio baba wa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa, haikuwa rahisi mjadala wa kuyapokea maelekezo ya IFM na World Bank, yakufanya mageuzi ya kiuchumi kwenye NEC haikuwa rahisi yalikuwa magumu, akasema jamani ee kama ni mkuki unanichoma mie, mbele mkuki, nyuma mkuki.

MAGEUZI YA KISIASA

Kikwete anasema mageuzi ya kisiasa Mzee Mwinyi aliunda tume ya Jaji Francis Nyalali, tume ile ilikuja na mapendekezo asilimia 80 walikuwa wanataka tubaki na mfumo wa chama kimoja, 20 wanasema twende mfumo wa vyama vingi chini ya uongozi wake uamuzi ukafanyika wachache wape, hapakuwa na uamuzi wa wengi wape, na hoja ikaja 20 sio kidogo!

Akaja na mfano hivi sisi tumejifungia ‘white house’ (Ikulu), wenzetu 20 wapo nje na madebe wanapiga na kila kitu tutakaa sawa sawa? Lakini la busara kuliko lote ilikua kama asilimia 80 imeonyesha imani na CCM tuingie kwenye mfumo wa vyama vingi, ikija kubadilika 80 wakasema twende kwenye mfumo wa vyama vingi na 20 tubaki chama kimoja maana yake kwa CCM tunakwenda kuondoka.

“Na busara ile chini ya Mzee Mwinyi ndio maana CCM itaendelea kutesa, jamaa wanasema, wanaongea CCM ipo pale pale mpaka leo na miaka inayokuja.

“Kiongozi mwenye hekima kwa jambo gumu anaongoza watu kufanya uamuzi wa busara na wenye  maslahi kwa nchi yetu,” amesema Kikwete

AVUNJA BARAZA LA MAWAZIRI

Kikwete anasema Hayati Rais Mwinyi alivunja Baraza la Mawaziri mara mbili, mara ya kwanza aliwaita  wote Mawaziri na Manaibu Mawaziri alikuja hakuonesha bashasha akasema nawashukuruni kwa mlivyonisaidia ila wenzangu naomba muende mkajiuzulu, eee!

“Tunatazamana wote tukajiuzulu eee! Akanyanyuka akaondoka, basi na sisi tukaondoka, kutoka nje hakuna magari madereva wameshaondoka kwa sababu tuliamini ni mkutano na ungechelewa kuisha waliwaruhusu madereva waondoke na magari.

Kwa vile wakati huo hakukuwa hata na simu za mkononi, haikuwezekana hata kuwaita madereva ili wawape usafiri wa kuondoka Ikulu, ikabidi watoke na kuanza kutembea kwa miguu, wakiwa wameongozana.

“Namshukuru Mzee Msuya (Cleopa) alikuwa Waziri wa fedha tukatembea mpaka ofisini kwake akatupa magari yakatupeleka, tukawa tunafikiria hivi tunaandikaje barua ya kujiuzulu.

Baada ya muda tukapata barua tusijiuzulu, baada ya muda tukapata barua wote tumefukuzwa ondokeni ofisini kakaeni nyumbani hadi mtakapoitwa tena, basi akaunda tena Baraza ndio nikawa Waziri kamili.

Mara ya pili alivunja baraza haikuwa kama mara ya kwanza safari ile, ilitangazwa tu kwenye taarifa ya habari Rais amevunja Baraza la Mawaziri.

“Rais Mwinyi alikwua jasiri, ninachosema kwa watanzani wenzangu tumkumbuke Mzee huyo ndio kiongozi aliyefikisha nchi yetu hapa ilipo, mtu mwema, hana makuu, ana huruma lakini ni dhabiti kwenye maamuzi

MWINYI KANIFIKISHA HAPA

Kikwete anamshukuru Mzee Mwinyi ndio alinianzishia safari yake ambayo ilimfikisha kwenye urais.

“Namshuru sana yeye ndio aliyenifanya hatimae kuwa Rais, kama nilivyosema matumaini yangu yalikua kuendesha akili yangu kwenye jeshi na kuendesha ujumbe kwenye chama. Alichokiona kwangu sijui lakini nimefika hapa nilipofika kwa ajili yake namshukuru.

Fundisho la Nne: Kikwete anasema funzo lingine alilolipata kwa Mzee Mwinyi ni kuwa jambo unaloliamini komaa nalo.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button