Kilimo himilivu; suluhu mabadiliko ya tabianchi
MABADILIKO ya tabianchi yamekuwa na athari kubwa kwa uzalishaji wa kilimo katika Mkoa wa Songwe, hususani kwa wakulima wadogo wanaotegemea mvua, hali inayoathiri upatikaji wa lishe bora kuanzia ngazi ya kaya.
Athari hizi zimejidhihirisha kupitia mabadiliko ya mifumo ya mvua, kuongezeka kwa joto, na kuenea kwa magonjwa na wadudu waharibifu wanaoathiri mazao ya chakula.
Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wilaya ya Mbozi, George Nipwapwacha, anasema wakulima wameathirika na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo kupungua kwa mavuno na kuongezeka kwa wadudu na magonjwa ya mimea.
Anatoa mfano wa Kijiji cha Ikomela kilichopo Kata ya Kilimampimbi ambacho miaka ya karibuni kimevamiwa na funza waharibifu wanaoshambulia mazao ya chakula aina zote yanayolimwa eneo hilo pamoja na kahawa.
Anasema mpaka sasa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Udhibiti wa Viuatilifu Tanzania (THPA) wanaendelea kufanya tafiti za kupata viuatilifu vitakavyo mtokomeza mdudu huyo.
Akielezea kuhusu hali ya mvua anasema miaka ya nyuma kwa wilaya ya Mbozi mvua zilikuwa zinaanza kunyesha kuanzia Septemba mpaka Mei, lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayochangiwa na shughuli za kibinadamu, mvua zinaanza kunyesha Novemba au Desemba na kuathiri uzalishaji wa chakula kuanzia ngazi ya kaya.
“Mfano msimu wa kilimo wa 2025, mvua zilisimama kunyesha kwa muda mrefu katikati ya mwezi Februari na kusababisha mazao mengi hasa zao la mahindi ambalo ni zao kuu la chakula kunyauka, huku wakulima wakiwa tayari wameweka mbolea ya kukuzia,” anasema Nipwapwacha.
Kwa upande wake Meneja wa kituo cha utafiti wa zao la kahawa TaCRI Nyanda za Juu Kusini, Dismas Panglas,
anasema tafiti walizofanya katika kituo cha hali ya hewa kilichopo Mbozi zimebaini toka mwaka 2012 mpaka
2025 kuna ongezeko la nyuzi joto 0.08 katika wilaya ya Mbozi.
Anasema pia wamenukuu kiwango cha juu cha nyuzi joto 34, ambazo hazijawahi kutokea katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.
“Madhara ya ongezeko la nyuzi joto hili tutarajie upotevu mkubwa wa mazao ambayo tumezoea kuyalima kwa sababu ya kukosekana kwa uwiano mzuri wa kiwango cha maji kinachotumiwa na mmea,” anaeleza Panglas.
Kutokana na athari hizo za mabadiliko ya tabianchi, shirika lisilo la kiserikali la MIICO wakishirikiana na Farm Africa, TMarc na SNV wanatekeleza mradi wa NOURISH chini ya ufadhili wa serikali ya Norway unaoelimisha wakulima kujikita katika kilimo himilivu ambacho kinaendana na mabadiliko hayo.
Meneja wa shirika lisilo la kiserikali la NIIMCO, Frimina Kavishe anasema kuna mazao ya chakula ya kimkakati yenye virutubisho ambayo ni suluhisho la athari za mabadiliko ya tabia nchi na kwamba wameanzisha mashamba darasa wakishirikiana na watalaamu wa kilimo ngazi ya kata na vijiji pamoja wakulima viongozi.
Frimina anayataja mazao ya kimkakati ya mradi wa NOURISH ambayo tayari wameanza kuyazalisha kupitia mashamba darasa hayo kuwa ni maharage lishe, mtama, alizeti, viazi lishe pamoja na mboga na matunda ambayo anadai kuwa yana virutubisho sita muhimu vinavyohitajika kwa watoto chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito na wanaonyonyesha.
“Lengo kubwa ni kutatua changamoto za mabadiliko ya tabia nchi, kutatua changamoto ya lishe kutokana na mkoa huu kuwa na kiwango kikubwa cha udumavu ambapo takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 31.9 ya watoto chini ya miaka mitano wana udumavu,” anasema.
“Lakini pia tunatoa elimu kuhusu usalama wa chakula huku tukihamasisha jamii kumpa nafasi mwanamke kushiriki kupanga bajeti kuanzia ngazi ya familia, sambamba na kuhamasisha kilimo mseto kinacho hitaji kuchanganya mazao na miti rafiki ambayo inatunza unyevu na kuzuia mmomonyoko wa udongo,” anaeleza Frimina.
Naye Ofisa Mnyororo wa Thamani wa Mradi wa NOURISH kutoka shirika la Farm Africa, Grace Changamike anasema wameanza utekelezaji wa mradi huo katika wilaya mbili za Mbozi na Momba kwa Mkoa wa Songwe kwa kushirikisha maofisa ugani wa kata, vijiji pamoja na wakulima viongozi.
Anasema katika mradi huo wakulima wanapata nafasi ya kujifunza kuhusu kilimo himilivu ambacho kina tija tofauti na mazao ambayo wameyazoea muda mrefu.
“Mpaka sasa kwa upande wa wilaya ya Momba tayari tumezifikia kata saba zenye wakulima 2460 waliopo kwenye viikundi ambapo wanaume ni 1,476 na wanawake 984.
Aidha, anasema mradi huo umezifikia kaya 656 zenye wajawazito na wanawake wenye watoto chini ya miaka miwili na kuzipatia elimu kila wiki kuhusu namna ya kutumia vema lishe bora.
Katika Wilaya ya Mbozi Changamike anasema tayari wamewafikia wakulima 5,280 katika kata 17 kwa awamu ya kwanza ya mradi huo.
“Kati yao wanaume 3,168 na wanawake 2,112, hawa wote tumewapatia elimu kupitia mashamba darasa tuliyoyaanzisha kwenye vijiji vyao tukishirikiana na maofisa kilimo kata na vijiji pamoja na wakulima viongozi,” anasema Changamike.
Mmoja wa wakulima wa kijiji cha Lwasho kata ya Myunga wilaya ya Momba, Furaha Kibona anasema awali walikuwa wakilima mazao ambayo wameyazoea lakini baada ya kujifunza kupitia mashamba darasa kuhusu kilimo himilivu, usalama wa chakula na Lishe bora kuanzia ngazi ya kaya wameanza kuzalisha mazao yanayoendana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo anayataja kuwa ni mtama, alizeti na kilimo mseto.



