Kiongozi wa upinzani akwama Yaoundé

YAOUNDE, CAMEROON : MGOMBEA Urais na Waziri wa zamani nchini Cameroon, Issa Tchiroma Bakary, amedai kuzuiwa kusafiri mapema leo wakati akijaribu kupanda ndege kuelekea Senegal kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Yaoundé.
Kupitia taarifa aliyoitoa kwenye mitandao ya kijamii, Tchiroma alisema kuwa alikuwa njiani kwenda kutoa heshima kwa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Cameroon, Ahmadou Ahidjo, aliyezikwa nchini Senegal alikofariki akiwa uhamishoni zaidi ya miongo mitatu iliyopita.
“Nilizuiwa kiholela kupanda ndege yangu kufuatia maagizo ya moja kwa moja kutoka kwa ofisi ya rais wa Jamhuri,” alisema Tchiroma katika taarifa hiyo.
Tchiroma ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha Cameroon National Salvation Front (CNSF), alieleza kuwa tukio hilo linaashiria kile alichokiita mivutano ya kisiasa. SOMA : Biya ajiimarisha kijeshi kabla ya uchaguzi
Hadi kufikia jana jioni, mamlaka ya Cameroon haikuwa imetoa kauli rasmi kuhusu sababu ya kumzuia Tchiroma kuondoka nchini, wala haijabainika kama hatua hiyo ilihusiana na lengo la safari hiyo au ni marufuku ya muda usiojulikana.



