Kishindo uzinduzi SGR Tanzania, Burundi

SERIKALI ya Tanzania na ya Burundi zimeunganisha nguvu na kuzindua ujenzi wa mradi mkubwa na kwanza Afrika Mashariki wa kuunganisha miundombinu ya Reli ya Kisasa (SGR).

Pia, zimefanikiwa kutimiza ajenda ya Umoja wa Afrika ya kuunganisha miundombinu bora ya usafiri ifikapo 2063, kufungua uchumi huku mradi huo ukitajwa kuwa kichocheo cha ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam.

Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye alizindua ujenzi wa mradi huo katika hafla iliyofanyika Musongati, Burundi jana.

Akizungumza wakati anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema nchi hizo zimeweka msingi imara wa mahusiano kwa kutekeleza mradi unaoziunganisha nchi hizo na kuimarisha usafiri na usafirishaji wa kisasa.

Alisema mradi huo ambao ni wa kwanza kutekelezwa kwa nchi za Afrika Mashariki utaimarisha na kupanua miundombinu ya usafirirshaji, kupunguza gharama na kuongeza ufanisi katika shughuli za kibiashara.

“Serikali zilikubaliana kujenga tawi la reli la Uvinza hadi Musongati kwa lengo la kuunganisha mgodi unaopatikana eneo hili na Bandari ya Dar es Salaam inayosafirisha mizigo mingi katika ukanda huu”.

Aliongeza: “Utekelezaji wa mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda zetu na ajenda za Umoja wa Afrika (AU) 2063 inayosisitiza kuunganisha nchi zetu kupitia miundombinu bora na ya kisasa ili kukuza mshikamano ustawi wa maendeleo ya wananchi”.

Mradi huu wa SGR kwa kipande cha kutoka Uvinza mkoani Kigoma hadi Musongati nchini Burundi una urefu wa kilometa 300, ikiwemo kilometa 240 za njia kuu na kilometa 60 za njia za kupishania na unatarajiwa kuwa na stesheni kupakia abiria na mizigo.

Katika kilometa 300 za mradi huo kipande cha saba kutoka Uvinza-Malagarasi kitakuwa na urefu wa kilometa 190 ambapo kilometa 156 njia kuu na kilometa 34 njia za kupishania na cha nane kinaanzia Malagarasi -Musongati chenye urefu kilometa 110,84 njia kuu na kilometa 26 njia za kupishania kilibuniwa mahsusi kwa ajili ya kubeba mizigo mizito na abiria.

Majaliwa alisema ujenzi wa reli hiyo unalenga kukuza uchumi kikanda kwa kuunganisha masoko yaliyopo nchini na yale ya nchi za nje na kuimarisha upatikanaji wa huduma muhimu za usafirishaji katika maeneo hayo.

Pia, reli hiyo itakuwa kichocheo cha maendeleo ya viwanda, kilimo, sekta ya madini na sekta nyingine za uzalishaji kwa kutoa huduma ya usafiri wa uhakika

“Reli hii itarahisisha usafirishaji wa bidhaa ikiwemo madini ya nikeli… hivyo basi nikeli hii itasafirishwa na reli yetu tuliyonayo, hivyo inakwenda kuchochea mahusiano, biashara na kufungua fursa zaidi kiuchumi.” alisema Majaliwa.

Kadhalika Majaliwa aliyataja mafanikio mengine kuwa ni kupunguza muda wa usafirishaji na gharama ya kusafirisha mizigo kutoka Dar es Salaam hadi Bujumbura kwa asilimia 40.

Alizitaka wizara zinazosimamia mradi huo kuhakikisha unakamilika kwa ubora na kwa wakati uliopangwa akiwasisitiza wawe wazalendo, wabunifu, waadilifu na kufanya kazi kwa kushirikiana.

Majaliwa aliishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kutoa ufadhili na kufanikisha upatikanaji wa wa mradi huo wa gharama ya Dola za Marekani bilioni 2.1 sawa na Sh trilioni 5.1 unaotarajia kuzalisha ajira za moja kwa moja 5,000.

Kwa upande wake, Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye alisema kuanza kwa ujenzi wa reli hiyo kutatibu shauku ya muda mrefu ya nchi hiyo kuwa na usafiri wa reli.

“Leo ni siku ya furaha sana kwetu. Tumepata jawabu la tangu enzi na enzi. Mwaka 1921, mradi huu ulianzishwa na Wabelgiji kisha wakaja Wajerumani lakini wakashindwa. Leo hii Tanzania na Burundi tumeweza,” alisema.

Alisema nchi yake imebarikiwa kuwa na madini mengi na kuna wakati aliitisha kikao cha wawekezaji kutoka nchi kadhaa. “Wengi walivutiwa na wakataka kuwekeza mara moja, lakini wakaniuliza, tukianza kuchimba madini ya nikeli, tutayasafirishaje?”

Aliongeza: “Hiyo changamoto ilitufanya tubungue bongo zetu na kutafuta suluhisho. Tunaishukuru sana Serikali ya Tanzania kwa kukubali kuungana nasi ili tuanze mradi huu muhimu. Tukitoka hapa, tunataka reli iunganishe hadi Kindu, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC). Na baada ya hapo, ifike Afrika Magharibi kwenye ufukwe wa Bahari ya Atlantiki kwani tunaamini njia hiyo itaharakisha kuleta maendeleo.”

Rais huyo alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufikia hatua kubwa za maendeleo.

Alisema amekaa muda mrefu nchini lakini kwa sasa akija anaweza kupotea.

“Magomeni napajua, Tabata na Vingunguti napajua, Mwenge napajua na Kinondoni nilishakaa lakini kwa sababu ya maendeleo yaliyopatikana, naweza kupotea. Tunamshukuru kwa uongozi wake imara,” aliongeza.

Rais huyo alizungumza kwa Kiswahili na kuamsha shangwe miongoni mwa wananchi waliohudhuria tukio hilo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button