Kiwanda chachochea ujasiriamali mazao kwa vijana, wanawake

Julai 31, 2023 Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alizindua Kiwanda cha kwanza cha kusindika matunda na mbogamboga kinachofahamika kwa jina la Mbeya Food Park.

Kiwanda hicho kimejengwa katika Kata ya Iyela, Halmashauri ya Jiji la Mbeya na ni sehemu ya juhudi za kukuza sekta ya kilimo na kuongeza thamani ya mazao ya wakulima. Kiwanda hicho ni miongoni mwa miradi mikubwa inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Programu ya AGRI-CONNECT.

Programu hiyo inalenga kuboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo, miundombinu ya barabara, upatikanaji wa huduma za kifedha, masoko na uboreshaji wa afua za lishe na maisha ya jamii za vijijini. Uendeshaji wa kiwanda hicho unafanywa na Kampuni ya Get Group Limited kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Mbeya kupitia ubia baina ya sekta binafsi na ya umma (PPP).

Uwekezaji na matokeo chanya
Uwekezaji huo unatajwa kuwa ni matokeo ya mazingira mazuri ya uwekezaji nchini yaliyoimarishwa kupitia sheria mpya ya uwekezaji ya mwaka 2022. Sheria hiyo iliyosainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali Desemba 2, 2022 imeongeza mvuto kutoka kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Mkurugenzi Mwenza wa Get Group Company Limited, Nelson Kisanga anasema kampuni yao iliamua kushirikiana na serikali kwa kuwa mazingira ya biashara yamekuwa bora zaidi. Anasema ujenzi wa kiwanda hicho umegharimu zaidi ya Sh bilioni moja, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mashine zinazotumika kusindika matunda na mbogamboga.

“Lengo kuu la kuanzisha kiwanda hiki ni kutoa ajira hasa kwa wanawake na vijana kupitia kilimo cha matunda na mboogamboga. Hii inahakikisha vikundi hivi vinanufaika na mnyororo mzima wa thamani,” anasema Kisanga.

Anaongeza kuwa kiwanda kinatoa huduma mbalimbali za usindikaji kama vile uchimbaji wa mafuta ya parachichi na alizeti, usindikaji wa viazi, ndizi na asali pamoja na utengenezaji wa bidhaa kama divai, viungo, virutubisho vya lishe na mboga zilizokaushwa.

Kwa sasa kiwanda kinahudumia zaidi ya watu 600, wengi wakiwa wajasiriamali wadogo wanaosindika mazao kwa matumizi ya kaya au biashara. Anasema usindikaji wa mazao unasaidia kupanua aina ya vyakula vinavyopatikana, hivyo kuboresha lishe kwa jamii.

Aidha, matumizi ya teknolojia ya uhifadhi yanasaidia kupunguza upotevu wa mazao na kuongeza usalama wa chakula. Anasema usindikaji wa mazao unasaidia pia kupanua wigo wa aina ya vyakula vinavyopatikana, hivyo kuboresha lishe kwa jamii.

Matumizi ya teknolojia ya uhifadhi pia yanasaidia kupunguza upotevu wa mazao na kuongeza usalama wa chakula. Vyanzo vinabainisha kuwa, zaidi ya vijana 20 wameajiriwa kwa mkataba wa kudumu huku wengine wakipata ajira za muda, hali inayochangia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana mkoani Mbeya.

Mabadiliko katika maisha ya vijana na wanawake
Ofisa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa kiwanda hicho, Gilbert Gosbert anasema uwepo wa kiwanda umebadili maisha yake. “Bila mtambo huu, nisingekuwa na kazi. Vijana wengi tumenufaika kwa kupata ajira za kudumu na za muda. Mbali na kazi, tunatoa mafunzo ya usimamizi wa masomo kwa wajasiriamali,” anasema Gilbert.

Anasema kiwanda hicho kimekuwa chachu ya mabadiliko katika Mkoa wa Mbeya kikiwapa wananchi fursa za kiuchumi na kijamii na kwamba, inaendelea kuwekeza katika miundombinu, mafunzo na masoko.

“Kiwanda hiki kina uwezo wa kuwa mfano wa kuigwa kukuza uchumi wa viwanda na kilimo Tanzania,” anasema Gilbert. Mmoja wa wafanyakazi katika kiwanda hicho, Neema Innocent anahamasisha wanawake kuutumia mtambo huo kama fursa ya kujitegemea kiuchumi.

“Mtambo huu umeniwezesha kifedha na kunifundisha ujuzi wa ujasiriamali… Nawashauri wanawake wengine wajitokeze, Rais Samia ametufungulia milango sasa ni zamu yetu kupiga hatua,” anasisitiza Neema.

Viongozi na wadau wamaendeleo
Diwani wa Kata ya Iyela, Musa Ismail anakiri kuwa kiwanda hicho kimeleta mageuzi ya kiuchumi kwa wakazi wake. Anashukuru serikali kwa kushirikiana na wadau wengine waliowezesha kujengwa kwa kiwanda hicho ambapo wananchi wengi hasa wanawake na vijana wameweza kuanzisha na kuendeleza biashara za usindikaji wa mboga, matunda na viungo.

“Kiwanda hiki kimeongeza ajira, kipato na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kata na Jiji kwa ujumla,” anasema. Ofisa Biashara katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Richard Salagata anasema mradi huo ni matokeo ya jitihada za Rais Samia katika diplomasia ya uchumi.

“Mbeya imekuwa mnufaika mkubwa wa miradi ya kimataifa. Zaidi ya viwanda 1,000 vimeanzishwa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake kati ya viwanda 3,778 vilivyopo kwa sasa,” anasema Salagata. Salagata anasema wataendelea kushirikiana na kiwanda hicho kuwajengea uwezo na mafunzo ya kibiashara wajasiriamali wanaojihusisha na usindikaji ili wapate tija katika biashara zao.

Bertha Mwaipopo aliyeanzisha biashara ya usindikaji wa viungo na sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Lintu Product and General Supply inayozalisha aina 16 za viungo na kuuza katika mikoa mbalimbali, anatoa mwito kwa wanawake wengine kuchangamkia fursa katika kiwanda hicho.

Anawataka wanawake kutopuuza fursa za usindikaji wa mazao ya kilimo kwani ni sekta yenye faida kubwa ikiwa itafanywa kwa mipango na usimamizi mzuri.

Programu ilivyowezeshamageuzi
Akizungumza katika hafla ya kufunga programu ya AGRI-CONNECT iliyofanyika kiwandani hapo Machi 6, 2025, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde anasema kiwanda hicho kilichowezeshwa kupitia programu hiyo kimewezesha wajasiriamali kuongeza thamani ya mazao yao na kuunganishwa na masoko.

“Ninawashukuru Umoja wa Ulaya (EU) kwa ufadhili huu. Sasa wajasiriamali wanaweza kuchakata mboga, matunda na viungo kwa urahisi,” anasema Silinde. Kwamba, kiwanda hicho kinatoa fursa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kupata masoko ya uhakika kwa bidhaa zao, ikiwa ni pamoja na maduka makubwa.

Hatua hiyo inawawezesha kuongeza uzalishaji na uboreshaji wa ubora katika bidhaa zao. Anaongeza kuwa, Kiwanda cha Mbeya Food Park kinachangia katika ukuaji na ustawi wa uchumi wa Mkoa wa Mbeya na taifa kwa ujumla kwa kuongeza thamani mazao ya kilimo, kuunda ajira na kuvutia uwekezaji katika kilimo na viwanda.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button