Kongani za viwanda Mtwara kukuza uchumi wa wananchi

“LENGO la serikali ni kwamba ifikapo mwaka 2030, asilimia 100 ya korosho yote inayozalishwa nchini ibanguliwe hapa nchini.”

“Maana yake ni kwamba, lazima tuwe na viwanda vya kutosha vya kubangua korosho nchini na hii si kwa korosho peke yake, bali na ufuta pia hivyo, lazima tuwe na viwanda hivi vya kuongeza thamani.”

Anasema Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dk Hussein Mohamed hivi karibuni alipotembelea Kongani ya viwanda katika Kijiji cha Maranje, Nanyamba mkoani Mtwara. Anaiagiza Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) kuendelea kuhamasisha watu, kampuni na taasisi mbalimbali kuwekeza katika kongani hiyo.

Kwa mujibu wa Dk Mohamed, serikali pekee yake haiwezi kuendeleza kongani hiyo ipasavyo, hivyo unahitajika uwekezaji kutoka sekta binafsi kufanikisha azma hiyo.

Katika ziara yake kutembelea Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI)-Naliendele, naibu katibu mkuu huyo anasema ili kufikia azima ya Tanzania kufikia uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050, kilimo ni moja ya sekta muhimu za mageuzi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Dk Hussein Mohamed akipokea taarifa ya mradi wa ujenzi wa kongani ya viwanda kutoka kwa mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Mangile Malegesi

“Hakuna mafanikio katika kilimo bila utafiti kwa hiyo, TARI mtakuwa sehemu kubwa na muhimu ya mageuzi ya nchi  hii kiuchumi kupitia utafiti,” anasema. Anaongeza: “Serikali imeainisha mazao 15 ya kimkakati na korosho ni miongoni mwa mazao hayo…”

“Tunataka tufikie uzalishaji wa tani milioni 1 ifikapo 2030 na TARI Naliendele mna nafasi kubwa mno ya ama kutuangamiza, au kutunyanyua,” anasema.

Kimsingi, serikali imedhamiria kuendelea kutekeleza kwa dhati agenda ya uchumi wa viwanda kwa kufanya uwekezaji wenye tija katika maeneo mbalimbali nchini. Kufikia azma hiyo, moja ya sekta muhimu ni viwanda ambavyo si siri, ni sekta nyeti katika kukuza uchumi wa nchi.

Kwa mujibu wa wataalamu wa mambo ya uchumi viwanda vina nafasi muhimu katika kufanya maisha ya Watanzania kuwa bora zaidi, kurahisisha upatikanaji wa soko la uhakika la malighafi zinazopatikana nchini pamoja na kutoa ajira kwa wananchi.

Haya yanakwenda sambamba na viwanda kuwezesha upatikanaji wa fedha za kigeni nchini. Kutokana na faida hizo
kupitia sekta ya viwanda, serikali inaendelea na ujenzi wa kongani ya viwanda katika Kijiji cha Maranje, Kata ya Mtiniko Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara.

Kwa hatua za mwanzo, kongani hiyo itakuwa na uwezo wa kubangua korosho tani 30,000. Hivi karibuni HabariLEO
lilizungumza na wananchi katika Halmashuri ya Mji wa Nanyamba likitaka kufahamu namna walivyopokea uwekezaji huo wa kongani katika eneo lao na namna watakavyonufaika na mradi huo.

Mkazi wa Kijiji cha Hinju, Daudi Mashaka anasema kitendo cha serikali kuleta uwekezaji huo ni moja ya njia za kulitafutia soko zaidi zao la korosho na mazao mengine. Anasema ni fursa kubwa pia kwa wananchi wa maeneo hayo na mkoa kwa jumla kujipanga kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kukuza vipato vyao.

“Tunaamini kabisa kuwa, kupitia uwekezaji huu wa kongani, zao letu la korosho litakuwa na tija kubwa zaidi kwa mkulima,” anasema. Daudi anaongeza: “Kitendo cha serikali kutuletea kiwanda kikubwa kama hiki, ni fursa kubwa wetu vijana na jamii kwa ujumla kupata ajira za muda mfupi na hata za muda mrefu.”

Dk Hussein Mohamed akitazama ramani ya mradi huo. (Picha zote na Sijawa Omary).

Mwananchi mwingine mkazi wa Kijiji cha Kitachi, Abdulaazizi Dodi anashukuru serikali akisema kiwanda hicho kitachochea zaidi maendeleo ya Wanamtwara. Dodi anasema pia kitasaidia kuongezea thamani zao hilo hali itakayowafanya wakulima wa korosho na wananchi kwa ujumla kunufaika zaidi kiuchumi kupitia kilimo cha zao hilo.

“Tunaposema uchumi mbadala wa korosho ghafi mfano bibo la korosho linatengenezwa siagi, juisi pamoja na bidhaa ningine nyingi tu,” anasema. Anaongeza: “Kwa hiyo niseme tu kwamba, uwekezaji huu mkubwa unaofanywa na serikali yetu tumeupokea kwa mikono yote miwili kwa sababu utakuwa mkombozi kwa jamii.”

Naye Zena Lihumbo wa Kijiji cha Chiwindi anasema: “Tunamshukuru sana Mama Samia (Rais Samia Suluhu Hassan) kwa kutuletea mradi huu mkubwa kwani hautanufaisha watu wachache tu, bali utanufaisha watu wengi wa
ndani na wa nje ya Mtwara.”

Anasema wao kama wanawake, kupitia uwekezaji huo watahakikisha wanashiriki kikamilifu katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi. Kwa mujibu wa Zena, hayo ni pamoja na kufanya biashara ya mamalishe na shughuli nyingine za kujiingizia kipato sambamba na kuendesha majukumu ya kifamilia kama vile kusomesha watoto.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa CBT, Mangile Malegesi anasema eneo linalofanyika uwekezaji huo wa kongani lina jumla ya hekari 1,572. Malegezi anasema eneo hilo linatarajiwa kuwa na viwanda zaidi ya 60
likigharimu takribani Sh bilioni 5.6 hadi kukamilika kwa mchakato wote wa ujenzi.

“Kwa kukamalika kwa mradi huu, tunatarajia sasa Mkoa wa Mtwara na ukanda mzima wa Kusini utachangamka zaidi kiuchumi,” anasema.

Anaongeza kuwa, ajira zitakazopatikana hapo hazitahusu watu wa Mtwara pekee, bali hata watu wengine kutoka nje ya mkoa huku sehemu kubwa wakiwa ni wanawake na vijana. Anasema: “Kwa kweli ajira nyingi zitapatikana katika
eneo letu hili la Maranje…”

Malegesi anataja faida mbalimbali zitazotokana na kongani hiyo kuwa ni pamoja na ajira za kawaida takribani 35,000 kwa kuwa watu watapata ajira za moja kwa moja. Nyingine ni uuzaji wa korosho na bidhaa zake badala
ya kuuza korosho ghafi. Hizi ni pamoja na maganda ya korosho na mafuta yanayotokana na maganda ya korosho.

“Kwa hiyo mkulima atanufaika na zao lake mara mbili ya kile anachokipata na serikali itapata mapato ya kutosha kwa sababu ile tozo iliyokuwa inaipata kwenye korosho ghafi sasa itapata mapato yanayozalishwa na viwanda,” anasema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button