Kuchapwa kwa vikongwe, wanamtandao watoa neno

MTANDAO wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi umepokea  kwa mshtuko mkubwa taarifa ya kucharazwa viboko wanawake wakongwe mkoani Tabora na kutoa mapendekezo matano ili kukomesha

Tayari Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum jana Desemba 15, 2022 aliielekeza ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa wa Tabora kwa niaba ya Kamishna wa Ustawii wa Jamii, kushirikiana na vyombo vya haki mkoani humo kuhakikisha wanafufua shauri la wazee hao waliochapwa viboko kwa tuhuma za kishirikina, ili mashahidi watoe ushahidi wao kuhusu kesi hiyo.

Hata hivyo, Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi katika taarifa yao iliyotolewa leo Desemba 16, 2022, imesema  pamoja na kuipongeza serikali kwa hatua ilizozichukua kufuatilia suala hilo  kupitia Wizara  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum; bado kuna  haja ya suala hilo kuwekewa msisitizo na hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi ya wanaokwamisha upatikanaji wa haki kwa ukatili mkubwa uliotendeka.

“ Tunatoa wito kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum; Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; pamoja na  Jeshi la Polisi Tanzania kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kufanya upelelezi kwa wale wote waliohusika katika tukio hili la kinyama na la kusikitisha,”imesema taarifa hiyo

Aidha, wameomba kuwarejesha wanawake hao katika makazi yao pamoja na kuwapatia ulinzi.

“Pia tunashauri suala hili lifuatiliwe na kushughulikiwa kwa uwazi ili wananchi wote waweze kurejesha imani ya utawala wa sheria na upatikanaji wa haki kwa viongozi na serikali kwa ujumla.” Imesema taarifa hiyo ya Wanamtandao na kuongeza

“Mtandao unaendelea kutoa wito kwa jamii kutovifumbia macho vitendo dhalilishi, vya kikatili, vya kinyama na vya uvunjifu wa haki kwa wanawake na jamii nzima, kuchukua hatua na kutoa taarifa kwa vyombo husika pindi vitendo hivyo vinapofanyika.” Imesisitiza

Tamko hilo la Wanamtando limekuja ikiwa ni siku moja baada ya kusambaa video  kulisambaa ‘clip ya video’  inayowaonyesha wanawake wakongwe wanne na binti zao wawili mmoja akiwa mjamzito, wamechapwa viboko wakiwa wamemwagiwa maji na kupunguzwa nguo mwilini.

Video hiyo ilionesha wanawake hao wakilalamika kitendo hicho ambacho kinadaiwa kufanywa na baadh ya watu kwa kushikiriana na Diwani wa Kata ya Kasisi, Wilaya ya Urambo, Mkoa wa Tabora kwa madai kuwa wanawake hao ni wachawi na washirikina ambao wamekuwa wakichukua vyakula vya watu kwa nguvu za kishirikina wakati wa usiku.

Wanawake hao walipatwa na kadhia hiyo wakiwa katika shughuli zao za kujipatia kipato ambapo kufuatia tukio hilo walipoteza mazao na vitu mbalimbali. Tukio hilo pia liliwasababishia maumivu makali ya mwili na viungo, limewadhalilisha wao binafsi, familia zao na jamii nzima.

“Mpaka taarifa hizi zinatufikia, tayari familia za wanawake hao zilikuwa zimelazimika kuhama makazi na kwenda kuishi maeneo mengine kwa kuogopa vipigo zaidi, kubomolewa nyumba zao na vitisho dhidi ya maisha yao ambavyo walivipata kutoka kwa Diwani huyo.  Mtandao unajiuliza, Je usalama wa hawa watu uko wapi? Mali zao walizoacha zipo salama? Huko walipo wamepewa ulinzi?” Imehoji taarifa ya Wanamtandao hao

Aidha, imesema vitendo hivyo vya kikatili ni mwendelezo wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu huku wanawake wakiwa ndiyo wahanga wakubwa wa matukio hayo hapa nchini, havipaswi kufumbiwa macho, havivumiliki na havikubaliki na wanavilaani  kwa nguvu zote.

“Taarifa hizi za viongozi kuhusishwa na vitendo vya ukatili na matumizi mabaya ya mamlaka hapa nchini zinazidi kuongezeka. Hivi karibuni katika kipindi cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, tulishuhudia binti mmoja aliyejulikana kama Florenencia Mjenda ambaye alieleza kupitia vyombo vya habari tukio la kupigwa na Mkuu wa Wilaya ya Songwe, mkoani Mbeya hadharani kwa kosa linalosemekana kukalia jukwaa kimakosa. …..; “Vitendo hivi vinaonekana kushika hatamu na vikikaliwa kimya vitaendelea kushamiri na kuota mizizi.

“Ni jambo la kutafakarisha sana ikiwa viongozi ambao wamepewa dhamana na serikali na wananchi kuwaongoza kwa kufuata sheria na miongozo wao ndiyo wanakuwa wa kwanza kuvunja sheria. Ukatili wa kijinsia haukubaliki wakati wowote na mtu yeyote awe kiongozi ama raia wa kawaida.

Taarifa hiyo imesema uthubutu wa kuendelea kufanya vitendo hivi hususan katika kipindi hiki cha kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia vinakasirisha na kukera na vinaonyesha upungufu wa maadili na uvunjwaji wa sheria ambao unafifisha jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali pamoja na wadau wa masuala ya haki za wanawake na binadamu kwa ujumla.

KUHUSU SHERIA

Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi unatambua vema kuwa kitendo cha kuchapa (mtu) mwanamke ni kutokuheshimu utu wa mwanamke na ni matumizi mabaya ya mamlaka ambayo ni  kinyume na Katiba na Sheria za Tanzania.

Mathalani  katika Ibara ya 12(i)i[i] ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasisitiza kuwa kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake. Vilevile, ibara ya 13(i)ii[ii] imeainisha umuhimu  wa usawa na haki bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.

Tanzania pia inatambua na kutekeleza maazimio ya Tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa ambalo linasisitiza chini ya Ibara ya 3 haki ya kuwa huru na kulindwa, vilevile Ibara ya 9 ya tamko hilo, inaeleza kuwa hakuna mtu anayepaswa kukamatwa kiholela na kuwekwa ndani au kulazimishwa kwenda uhamishoni.

Vilevile, kitendo cha kujichukulia sheria mkononi, kujeruhi na kusababisha madhara ni kosa la jinai sawasawa na  kifungu cha  225 na kifungu cha 228(a) cha sheria ya Kanuni ya Adhabu/ Penal Code [CAP. 16 R.E. 2022]

Aidha, kanuni kuhusu maadili ya madiwani zimeweka bayana umuhimu wa kuheshimu na kuzingatia sheria kwa madiwani ikiwa ni pamoja na kuendesha shughuli zao kufuatana na dhamana waliyopewa na wananchi.[iii]

[i] Ibara ya 12-

(1) Binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa.

(2) Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.

[ii] (1)Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki,

bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.

(2) Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake.

(3) Haki za raia, wajibu na maslahi ya kila mtu na jumuiya ya watu yatalindwa na kuamuliwa na Mahakama na vyombo vinginevyo vya Mamlaka ya Nchi vilivyowekwa na sheria au kwa

 [iii] Kanuni za maadili ya madiwani Kuzingatia haki na malengo yaliyowekwa na kuongozwa na ukweli na ushauri wa kitaaluma utakaotolewa na menejimenti ya Halmashauri na kuepuka kusukumwa na itikadi pamoja na hisia  binafsi wakati wa kujadili na kuamua masuala yanayohusu ustawi na maendeleo ya wananchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button