Kutuma maombi Bodi ya Mikopo mwisho Agosti 31

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa ELimu ya Juu (HESLB) imesema dirisha la maombi ya mikopo na ufadhili wa masomo kupitia Ufadhili wa Masomo wa Samia kwa mwaka 2025/2026, litafungwa Agosti 31, 2025.
Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha HESLB ilisema wanafunzi wenye uhitaji na sifa ambao hawajakamilisha maombi yao wanapaswa kukamilisha ili kuepuka msongamano wa dakika za mwisho na hakutakuwa na muda wa nyongeza.
“Tunawakumbusha waombaji wa mikopo na Samia Scholarship kwamba dirisha litafungwa Agosti 31, 2025 na hakutakuwa na muda wa nyongeza,” ilieleza taarifa hiyo.
Ufadhili wa masomo wa Samia ni programu ya ufadhili wa masomo unaotolewa chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa wanafunzi 1,000 waliopata ufaulu wa juu katika mitihani ya taifa ya kidato cha sita katika tahasusi za sayansi za PCB, PCM, CBG, PGM, CBA, PMC na CBN.
Ufadhili huo hugharamia masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wanaodahiliwa katika fani za teknolojia, uhandisi, hisabati na tiba kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa na wasimamizi wa ufadhili huo HESLB kulingana na muda wa kati ya miaka mitatu hadi mitano kulingana na programu husika walizodahiliwa.
Kadhalika, ufadhili huo unajumuisha ada ya mafunzo, posho ya chakula na malazi, vitabu na viandikwa, mahitaji maalumu ya vitivo, mafunzo kwa vitendo, utafiti vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na bima ya afya.
Kwa mujibu wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya 2025/26 serikali imejipanga kuongeza idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu kutoka 245,314 mwaka 2024/25 hadi wanafunzi 252,773 mwaka 2025/26 ikiwemo wanafunzi wa mwaka wa kwanza 88,320 na wanaoendelea 164,453.
Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni jijini Dodoma Mei, 2025, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema serikali itaendelea kutoa ufadhili kwa wanafunzi 2,630 wenye ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi kupitia Samia Scholarship, kati ya hao wanafunzi wa mwaka wa kwanza ni 1,220, shahada za umahiri wanafunzi 80 na wanafunzi wanaoendelea 1,330
Alisema pia serikali itaendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 50 wenye ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi hususani wanafunzi wa kike waliohitimu mitihani ya kitaifa ya kidato cha sita na shahada za awali kupitia Chuo Kikuu Dar es Salaam.