Lambert Vissot: Vifaa vya kisasa muhimu uchimbaji madini

LAMBERT Vissot, maarufu kama “The Gem Hunter,” ambaye ni mtaalam mashuhuri katika uchimbaji madini ya vito amesema kinachowezesha mafaniko makubwa katika uchimbaji madini ya vito ni uwepo wa vifaa vya kisasa vyenye uwezo mkubwa.

Vissort anaongoza shughuli za uchimbaji madini kupitia Kampuni ya Ruby International Limited yenye tawi lililopo Bangkok nchini Thailand inayomilikiwa na Mbunge wa Ulanga mkoani Morogoro, Salim Hasham.

Akizungumza na HabariLEO, Vissot amesema shughuli zote za uchimbaji na uuzaji wa madini ya spinel nyekundu na pinki unategemea zaidi vifaa vya kisasa na katika hilo wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa na hata katika kufikia malengo makubwa ya kampuni.

“Kuna utaalamu mkubwa ambao unatumika katika kufanikisha hilo na lazima uwe na mitambo na vifaa vya kisasa, na katika hilo tumefanikiwa sana kwenye eneo letu,” amesema Vissot ambaye ni raia wa Ufaransa.

Amesema licha ya kuwa na vifaa vya kisasa, ila uzoefu wake kwa miaka mingi wa kugundua madini ya aina hiyo, ni silaha nyingine anayojivunia kuwa nayo ambapo kwa kiasi kikubwa imewezesha kufikia mafaniko yake binafsi na kampuni.

Hata hivyo ameshauri kampuni zingine zenye malengo makubwa kutumia vifaa vya kisasa ili kufikia mafanikio wanayohitaji. Amesema kampuni bado inaendelea kuangalia namna ya kuongeza zaidi vifaa vingine ili kuendana na kasi ya teknolojia.

“Hata hatujamaliza bado tunaendelea kuangalia namna ya kuendana na kasi ya teknolojia na kuona kwa kiasi gani shughuli hizi zinahitaji vifaa zaidi vya kisasa,” ameongeza Vissot.

Aidha amesema sifa yake ya kupata madini bora kutoka katika maeneo yenye ubora wa kipekee, ni sababu ambayo inafanya kampuni hiyo kupitia tawi lake nchini Thailand kujivunia mafaniko waliyonayo kwa sasa.

“Nina uzoefu mkubwa sana na hili ni suala ambalo linanifanya nijivunie binafsi hata kampuni pia kwa hiyo tunaenda vizuri, kampuni inachimba na kuuza madini nje ya nchi pia,” ameongeza Vissot.

Habari Zifananazo

Back to top button