Latra kutoa vibali maalumu mabasi 150 Dar

DAR ES SALAAM; MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetoa nafasi ya maombi ya vibali 150 kwa wasafirishaji Mkoa wa Dar es Salaam wenye mabasi maarufu ‘daladala’ yanayoweza kubeba abiria kuanzia 26 na kuendelea kwa kipindi cha miezi mitatu.
Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo amesema mabasi hayo yanatarajiwa kufanya kazi kutoka Mbezi Luis kupitia barabara ya Kimara kwenda Posta, Mnazi Mmoja, Muhimbili na Makumbusho.
Suluo alisema hiyo imetokana na marekebisho yanayotarajiwa kufanyika katika miundombinu ya vituo vya mabasi yaendayo haraka maarufU ‘Mwendokasi’ iliyoharibika ambayo imepelekea changamoto za usafiri wa mabasi hayo kwa njia inayotoka Kimara kuelekea katika maeneo tajwa.
“Tuna nafasi 150 kwa mabasi yenye uwezo wa kubeba abiria 26 na kuendelea atakayewahi tutampa nafasi ya mwanzo, hii inatokana na changamoto za usafiri wa mabasi yanendayo haraka kwa njia ya BRT1 ya kwenda huko Kimara na hivi vibali tutavitoa kwa kipindi cha miezi mitatu,” alisema Suluo.
Aliongeza kwa upande wa barabara ya BRT2 yaani upande wa safari za Mbagala alipewa mwekezaji Mofat na hakuna uharibifu mkubwa wa miundombinu ya kukatia tiketi na kuingia, hivyo marekebisho yake yatafanyika kwa muda mfupi na mwekezaji atarudi kuendelea kutoa huduma.
Alisema hawana matangazo ya vibali kwa ajili ya njia hiyo kwa sababu kuna mabasi yanayopita njia ya pembeni ambayo yataendelea kutoa huduma, kwani ni kituo kimoja cha Mbagala Zakheim ndicho chenye uharibifu mkubwa na baada ya marekebisho watarudi kutoa huduma.
Pia, Suluo alisema maombi ya vibali hivyo ni kwa wale wanaohitaji na yatafanyika kupitia mfumo wao wa Usimamizi wa Taarifa za Reli na Barabara (RRIMS).
Katika hatua nyingine Latra imetekeleza agizo la Mkuu wa Dar es salaam, Albert Chalamila lililowataka kuhakikisha usafiri kwa kwenda mikoani kuanzia Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli kurejea kama kawaida.
HabariLEO mapema jana asubuhi ilishuhudia baadhi ya mabasi kuelekea katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini yaani Arusha, Kilimanjaro na Tanga yameanza kufanya kazi.



