Leila Khamis : Mwanamke pekee mgombea urais Zanzibar

LEILA Rajab Khamis ni miongoni mwa wagombea 11 wa urais wa Zanzibar, akiwa mwanamke pekee akipeperusha bendera ya Chama cha National Convention for Construction and Reform (NCCR-Mageuzi). Anasema amejipanga kufanya mageuzi makubwa ya maendeleo ya Zanzibar endapo atapewa ridhaa ya kuongoza Zanzibar.

Kwa mujibu wa Leila, anafurahi kwamba Tanzania ipo katika kipindi muhimu cha mageuzi ya kisiasa yanayofungua milango kwa wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi wa ngazi za juu, kwani zama za mfumo dume zimekwisha. Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kibandamaiti, Unguja anatangaza vipaumbele 11 alivyopanga kutekeleza katika kipindi cha miaka mitano akipewa ridhaa na kuongoza Zanzibar.

Leila anasema miongoni mwa vipaumbele vyake ni pamoja na kuimarisha uchumi wa Zanzibar, uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuzalisha ajira nyingi za vijana na mikopo nafuu kwa makundi ya wanawake.

Anasema kipaumbele cha kwanza ni kuimarisha uchumi wa buluu kwa kutumia Bahari ya Hindi kupitia fursa mbalimbali, ikiwemo uvuvi wa bahari kuu. Anasema hadi sasa licha ya juhudi kubwa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika uchumi wa buluu, bado uvuvi wa bahari kuu na fursa zilizopo katika eneo hilo hazijatumika kikamilifu.

Kwa mujibu wa Leila, akichaguliwa serikali chini ya uongozi wake itawapa wavuvi boti za kisasa zenye uwezo wa kufika maeneo yenye kina kikubwa cha maji ili kuvua samaki wanaopatikana maeneo hayo, wakiwemo samaki aina ya Jodari wenye kipato kikubwa na maarufu kutumika katika hoteli za kitalii.

“Nimejipanga kuimarisha sekta ya uchumi wa buluu na kuona inaongoza katika kuchangia pato la taifa ambapo katika kuwawezesha wavuvi kuvua katika maeneo ya bahari kuu, tutawapatia boti za kisasa zitakazowafikisha eneo hilo,” anasema.  Aidha, anasema ataimarisha sekta ya kilimo na kuhakikisha inachangia ajira kwa kundi la vijana kupitia kilimo kwa kutumia mbinu za kisasa na vifaa, yakiwemo matrekta.

Anasema sekta ya kilimo ilivyo sasa, haiwezi kuwa kimbilio kamili la vijana kwa kuongeza ajira. Leila anasema hali hiyo ndiyo inafanya vijana wengi kukimbia kilimo na kutafuta ajira serikalini, kwani wanaona kilimo hakiwezi kuwapa ajira kama wanavyotarajia.

“Sekta ya kilimo hatujaitumia kikamilifu kama eneo moja muhimu la kuzalisha ajira kwa vijana… nikichaguliwa tutawakusanya vijana na kuwapa mikopo kulima mboga mboga na kuwaunganisha na mnyororo wa thamani katika masoko ya uhakika, hata kupitia sekta ya utalii,” anasema. SOMA: Akili unde isichafue pambazuko la wanawake kuchaguliwa 2025

Leila anataja vipaumbele vingine kuwa ni kuwezesha wanawake kutimiza azma yao ya kuwa wajasiriamali katika sekta ya biashara. Anasema akichaguliwa kuwa rais, serikali itawapa mikopo isiyokuwa na riba. Kwa mujibu wa Leila, utafiti unaonesha wanawake wengi huchukua mikopo yenye riba na masharti magumu isiyowafikisha katika malengo yao ya kuwa wajasiriamali ili kukabili umasikini, badala yake inawakwamisha kiuchumi na kimaisha.

Anasema akichaguliwa kuingia madarakani na wananchi, ndiko kutakuwa mwisho wa mikopo ya namna hiyo iitwayo ‘kausha damu’ na wanawake watainuliwa kiuchumi kwa mikopo rafiki itakayowaondolea umaskini na utegemezi. Kipaumbele kingine kwa mujibu wa Leila ni kuimarisha huduma za jamii, ukiwemo ujenzi wa hospitali za mikoa zikiwa na hadhi na sifa za kutoa huduma kwa wajawazito na watoto, hatua itakayoepusha vifo vinavyotokana na kundi hilo.

Leila anampongeza Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi kwa ujenzi wa hospitali za wilaya 11 na moja ya Mkoa wa Lumumba, akisema akichaguliwa ataunga mkono juhudi hizo. Anasema katika kipindi cha uongozi wake wa miaka mitano, Dk Mwinyi amefanya kazi kubwa kuimarisha huduma za afya kwa akina mama na watoto na hivyo kukaribia malengo endelevu ya dunia ya kupunguza vifo vinavyotokana na kundi hilo, ifikapo mwaka 2030.

Anasema wanaunga mkono kasi ya ujenzi wa shule za ghorofa katika ngazi ya msingi hadi sekondari, hatua iliyoanza kuleta matokeo chanya ya ufaulu kwa wanafunzi wa shule hadi kuingia vyuo vikuu. “Chama changu cha NCCRMageuzi tunaunga mkono kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Rais Dk, Hussein Mwinyi kwa kasi ya ujenzi wa miradi ya jamii, ikiwemo ya shule na hospitali na tukichaguliwa tutaendeleza suala hilo,” anasema.

Anataja maeneo mengine ya vipaumbele vyake kuwa ni pamoja na kuimarisha taasisi za utafiti katika sekta mbalimbali, zikiwemo za uvuvi, kilimo pamoja na mifugo ili kuhakikisha sekta hizo zinaleta mageuzi makubwa ya maendeleo na kuongeza ajira. Anasema hadi sasa, miongoni mwa sekta zilizo nyuma ni pamoja na mifugo. Licha ya kuwepo kwa soko la nyama na maziwa pamoja na mayai katika sekta ya utalii, bado wafugaji wapo nyuma huku wakitumia mbinu za kizamani.

Anasema utafiti unaonesha kwamba kwa asilimia 60 Zanzibar inategemea kuingiza nyama kutoka Tanzania Bara pamoja na mayai hadi maziwa ambayo hata hivyo, hayatoshelezi kwa matumizi ya hoteli za kitalii. Anasema akichaguliwa, anakusudia kusomesha wataalamu wengi zaidi katika sekta hiyo pamoja na madaktari bingwa wa mifugo, kuiondolea Zanzibar utegemezi wa mahitaji hayo.

“Suala la utafiti katika mifugo, kilimo na uvuvi wa bahari kwa ajili ya mahitaji ya mifugo na nyama, tutalipatia kipaumbele cha kwanza, ikiwamo kusomesha vijana wengi zaidi ili kupata wataalamu katika sekta hizo na hivyo vijana kujiajiri,” anasema.

Leila anawahimiza wanawake kuendelea kuthubutu kuwania nafasi za juu za uongozi, kwani hakuna lisilowezekana. Anavitaka vyama vyingine vya siasa kutoa nafasi zaidi kwa wanawake kugombea nafasi ya juu ya uongozi wa kisiasa. Leila anatoa mfano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimempitisha Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD) kimempitisha Mwajuma Mirambo kugombea urais, huku mgombea mwenza akiwa ni Mashavu Alawi Haji ambao wanaendelea na kampeni. Anahimiza, “Vyama vya siasa vifungue milango kwa wanawake na kuwaamini katika nafasi za juu za uongozi, zikiwemo za urais na kutoa mfano chama chake ambacho kimemteua Evaline Musisi kuwa mgombea mwenza wa nafasi ya urais wa muungano wa Tanzania kupitia NCCRMageuzi.”

Leila anatumia nafasi hiyo kuzipongeza taasisi na asasi mbalimbali i za kiraia, kikiwamo Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA)- Zanzibar chini ya mradi wa kujenga uwezo wa uongozi kwa wanawake. Anasema mradi huo wa TAMWA umewapa mafunzo yaliyowajengea ujasiri wa kujenga hoja zaidi katika majukwaa ya kisiasa.

“Nitumie nafasi hii kukipongeza kuwapongeza TAMWA Zanzibar kwa kutukusanya na kutupatia mafunzo yaliyotusaidia kwa kiasi kikubwa kwa kutujengea uwezo na uthubutu wa kujenga hoja katika majukwaa ya kisiasa katika kipindi cha mikutano ya kampeni,” anasema Leila.

TAMWA Zanzibar kimekuwa kikitekeleza mradi wa kujenga uwezo kwa wanawake kugombea nafasi mbalimbali za uongozi chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Norway nchini Tanzania, uliowajengea uwezo wanawake zaidi ya 10,000 kwa nyakati tofauti kuhusu mbinu za uongozi na kugombea kupitia majimbo ya uchaguzi.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button