Lyra in Africa yaongeza nuru mafunzo kidigitali, Iringa na Dodoma

IRINGA: Walimu 20 wa shule 10 za sekondari za Iringa na Dodoma wamejengewa uwezo wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) kwa ajili ya kufundishia na kujifunza, kupitia mradi unaoratibiwa na shirika la Lyra in Africa.

Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyofanyika mjini Iringa yamelenga kuongeza ufanisi wa ufundishaji kwa njia ya kidijitali, sambamba na kuwaandaa wanafunzi kupata maarifa na ujuzi wa kisasa unaohitajika katika dunia ya sasa ya teknolojia.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mratibu wa Elimu Jumuishi Kidigitali kutoka shirika hilo, Konzo Ikweta, alisema mafunzo hayo yamewapa walimu mbinu mbalimbali ikiwemo namna ya kuwa raia wema mtandaoni kwa kuepuka kuchapisha au kusambaza maudhui yasiyofaa, pamoja na kutumia vifaa vya kidijitali kama simu janja, kompyuta na programu (apps) mbalimbali za kujifunzia na kufundishia.

“Tunawajengea walimu uwezo wa kutumia teknolojia kwa ubunifu katika ufundishaji ili waweze kuwasaidia wanafunzi wao kujifunza kwa njia ya kisasa, kwa ufanisi na kwa kushirikiana zaidi,” alisema Ikweta.

Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Afisa Taaluma wa Mkoa wa Iringa, Martha Lwambano, aliwataka walimu hao kutumia ujuzi walioupata kuleta mabadiliko si tu katika shule zao bali pia katika shule jirani.

“Walimu bora ni wale wanaotumia ujuzi wao kuwasaidia wengine. ICT ni nyenzo muhimu ya kuwajengea wanafunzi wetu uwezo wa kukabiliana na changamoto za dunia ya sasa,” alisema Lwambano.

Walimu walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kunufaika sana na mafunzo hayo.

Mwalimu Musa Mgongo kutoka Shule ya Sekondari Msanga wilayani Chamwino mkoani Dodoma alisema mafunzo hayo yamempa ujasiri zaidi katika ufundishaji na yataongeza uelewa wa wanafunzi wake kwa kasi.

Naye Mwalimu Aziza kutoka Shule ya Sekondari Mseke wilayani Iringa alisema ICT imemrahisishia kufundisha somo la Fizikia, ambalo kwa muda mrefu limekuwa likihitaji mbinu za ubunifu kufikisha uelewa kwa wanafunzi.

Katika kuhakikisha mazingira ya kujifunzia kwa njia ya kidijitali yanaboreshwa, Lyra in Africa imetoa jumla ya kompyuta 33 kwa kila shule—ikiwa ni kompyuta 30 kwa ajili ya wanafunzi na tatu kwa walimu.

Shule zinazofaidika na mradi huu ni pamoja na Mseke, Nyang’oro, Ilambilole, Maduma, Mlowa, Ifwagi, Lulanzi, Mazombe na Lundamatwe (mkoani Iringa), pamoja na Shule ya Sekondari Msanga (mkoani Dodoma).

Mradi huu ni sehemu ya juhudi za shirika hilo kuinua ubora wa elimu kwa kutumia teknolojia ya kisasa, na kuweka msingi madhubuti kwa vijana wa Tanzania kuingia katika soko la ajira la kidijitali.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button