M23 Yatuhumiwa Kuua 169 DRC

KINSHASA, DRC : UMOJA wa Mataifa umesema kuwa watu 169 wameuawa mwanzoni mwa mwezi huu kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na waasi wa M23 dhidi ya raia na wakulima katika eneo la Rutshuru, jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia Haki za Kibinadamu nchini humo (UNJHRO), operesheni hiyo ya M23 ilianza Julai 9 na kusababisha vifo hivyo vya raia wasio na hatia.SOMA:Watu 50 wapoteza maisha DR Congo
Kiongozi wa kundi hilo la waasi, Bertrand Bisimwa, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa wataanzisha uchunguzi wa ndani kuhusu madai hayo, lakini alidai ripoti hiyo huenda ni sehemu ya “kampeni ya udanganyifu”.
Matukio hayo yanajiri wakati Marekani, chini ya utawala wa Rais Donald Trump, ikiongoza juhudi za upatanisho kati ya DRC na Rwanda, zikilenga kuweka mazingira bora ya ushirikiano wa kiusalama na uwekezaji kwenye sekta ya madini yenye thamani ya mabilioni ya dola.