Maadili na haki za binadamu: Mvutano wa aina yake Afrika

MIJADALA kuhusu uhuru wa maamuzi na maadili barani Afrika inazidi kupamba moto, na Tanzania iko katikati ya mvutano wa kitamaduni wa kimataifa. Swali kuu linabaki: Nani anaamua jamii iishi vipi?
Kwa Umoja wa Ulaya (EU), jibu ni moja — haki za binadamu ni za wote, na usawa wa watu wenye mwelekeo wa jinsia au utambulisho wa kijinsia tofauti na ule wa kawaida wa kijamii unapaswa kulindwa kila mahali. Kwa Tanzania, viongozi na chama tawala CCM, jibu linapatikana katika misingi ya maadili, mila, na utamaduni wa kizazi kwa kizazi.
Mnamo Januari 2025, Huduma ya Utafiti ya Bunge la Ulaya ilisisitiza msimamo wa EU wa kuendeleza haki za jinsia na mwelekeo wa kijinsia duniani. Hata hivyo, ilikiri changamoto kwamba makubaliano na mataifa ya Afrika mara nyingi hayaelezi wazi masuala ya kundi hilo ili kuepuka mgongano wa kisiasa.
Wakosoaji nchini Tanzania wanaona hatua hiyo kama njama ya kifedha kupitia miradi ya mashirika yasiyo ya kiserikali, ikipuuza mahitaji muhimu kama afya, barabara na elimu.
Rais Samia Suluhu Hassan, alipowasilisha Sera ya Mambo ya Nje mwezi Mei 2024, alionya wanaharakati wa kanda wasiingilie mambo ya ndani ya nchi. “Tusiruhusu Tanzania iwe shamba la bibi kwa kila anayepita kutoa tamko,” alisema.
Wakati huohuo, ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ya 2024 ilionya kuhusu kupungua kwa uhuru wa kiraia na ongezeko la vitisho kwa wanaharakati na makundi yaliyotengwa, ikihimiza serikali kuoanisha sheria na viwango vya kimataifa. Serikali ilipinga ikisema ripoti hizo zinachochewa na ajenda za nje zinazotishia amani ya taifa.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, alisisitiza kwamba kurejesha maadili ni jukumu la jamii nzima. “Kila taasisi inapaswa kushiriki katika kuimarisha maadili ya taifa,” alisema, akieleza kuwa wizara yake inaendeleza mwongozo wa malezi ya watoto unaolinda maadili ya Kitanzania.
Katika muktadha wa Kiafrika, familia ni zaidi ya wazazi na watoto; ni msingi wa utamaduni na nidhamu ya kijamii. Mpango wa Maendeleo wa Halmashauri ya Kilombero (2021–2026) unasema kuporomoka kwa familia kunaleta kuporomoka kwa maadili na milango kwa ushawishi wa nje.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza kwenye Maulid Kitaifa Tanga, alisema Tanzania imejengwa juu ya misingi ya amani, uzalendo na maadili mema. “Maisha ya Mtume yanatufundisha kuishi kwa maadili na kutegemea Mungu,” alisema, akisisitiza kulinda amani kama zawadi ya kiungu.
Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ali, aliwataka viongozi wa dini kuimarisha mahubiri dhidi ya vitendo vinavyohatarisha amani, akisema: “Amani si hiari, kila mmoja ana wajibu wa kuilinda.”
Kwa serikali, maadili si suala la kidini tu bali ni msingi wa usalama wa taifa. Ndiyo nguzo ya ibada, maisha ya kila siku, na maendeleo.
Mjadala huu umeingia pia katika siasa. Wagombea wa upinzani, kama Hassan Almas wa NRA na mgombea wa ADC, wameahidi sheria kali zaidi dhidi ya ushoga — ishara kuwa hoja hii imekita mizizi kwenye uwanja wa kisiasa.
Tanzania inaungana na mataifa mengine ya Afrika kama Ghana na Uganda, yanayopinga kile kinachoitwa “uenezi wa tamaduni za Magharibi.” Kwa CCM, kulinda amani na maadili ya ndani ni ushahidi wa ufanisi wa misingi ya taifa.
Kutoka falsafa ya Ujamaa ya Nyerere, misimamo ya Magufuli, hadi diplomasia ya Samia, msimamo unabaki uleule — Tanzania inaamua yenyewe jinsi jamii yake inavyoishi.
Na hivyo swali linaendelea kuzungumzwa kwenye ofisi, makanisa, misikiti na vijijini kote: Nani anaamua jamii iishi vipi?