Mabadiliko Sheria ya Madini yawabeba Watanzania
ARUSHA: MABADILIKO ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 yametoa fursa kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali madini.
Hayo yamesemwa leo Mei 22, 2024 na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde katika ufunguzi wa Jukwaa la Tatu la Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini linaloendelea kwenye Ukumbi Kimataifa wa Mikutano AICC jijini Arusha.
Mavunde amesema, katika mabadiliko hayo suala la ushirikishwaji wa Watanzania limepewa kipaumbele ili kuhakikisha wawekezaji wote wanaojihusisha katika mnyororo wa uzalishaji na biashara ya Madini wanatoa kipaumbele kwa Watanzania.
Isome pia: https://habarileo.co.tz/changamkieni-fursa-sekta-ya-madini/
“Marekebisho ya mwaka 2017 ya Sheria ya Madini, yalipelekea kutungwa kwa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za Mwaka 2018 ili kuweka usimamizi thabiti katika utekelezaji wa masuala ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini nchini,”amesema Mavunde na kuongeza
“Kulikuwa na malalamiko mengi, Watanzania walikuwa ndugu watazamaji mpaka vyakula vilikuwa vinatoka nje, lakini baada ya mabadiliko ya sheria ya mwaka 2017 ushirikishwaji wa Watanzania umekuwa mkubwa sana sambamba na kushika nafasi za juu za uongozi kwenye kampuni za madini,”amesema.
Amesema, katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Machi, 2024, Wizara kupitia Tume ya Madini ilipokea na kupitia jumla ya mipango 801 ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika shughuli za Madini sawa na ongezeko la asilimia 57 ikilinganishwa na mipango 510 iliyopokelewa katika kipindi kama hicho kwa Mwaka wa Fedha uliopita.
“Hii ni wazi kuwa mwamko wa Watanzania katika kushiriki fursa zilizopo kwenye Sekta ya Madini unakua kwa kasi,”amesema
Amesema Wizara kupitia Tume ya Madini imeendelea kuhakikisha kuwa Watanzania wanapatiwa kipaumbele katika fursa za ajira zinazozalishwa katika migodi mikubwa na ya kati ya uchimbaji madini hapa nchini.
Mavunde amesema hadi kufikia Machi, 2024 jumla ya ajira rasmi 19,358 zilizalishwa katika migodi hiyo ambapo ajira 18,853 sawa na asilimia 97 zilitolewa kwa Watanzania na ajira 505 sawa na asilimia 3 zilitolewa kwa wageni.