Madaktari kanda ya ziwa wafundwa

MWANZA: MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umeendesha mafunzo kwa madaktari kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Mwanza, yamelenga katika kuwaongezea wataalamu hao weledi katika kufanya tathmini ya ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wafanyakazi wanaopatwa na changamoto hizo.
Akifungua rasmi mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, alisisitiza umuhimu wa madaktari kupata uelewa wa kitaalamu kuhusu masuala ya afya ya wafanyakazi, akieleza kuwa ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha haki za wafanyakazi zinazingatiwa kupitia tathmini sahihi za kitabibu.
“Serikali inatambua mchango mkubwa wa WCF katika kulinda ustawi wa wafanyakazi, aliongeza kuwa mafunzo haya yatawawezesha madaktari kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu namna ya kufanya tathmini ya ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi jambo litakalosaidia kupunguza changamoto za utofauti wa maamuzi ya kitabibu, hivyo kulinda nguvu kazi ya taifa,” alisema.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Anselim Peter, alibainisha kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wataalamu wa afya katika kuhakikisha wafanyakazi wanapata huduma kwa wakati, kwa ubora na kwa usahihi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF Dk. Abdulsalaam Omary alisema kuwa dhamira ya WCF kuongeza idadi ya madaktari wanaopata mafunzo ya aina hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.
Mmoja wa washiriki wa Mafunzo hayo Dk. Pius Kagoma amepongeza jitihada za WCF, akieleza kuwa mafunzo hayo yanawajengea uwezo wa kufanya tathmini kwa kuzingatia viwango ambapo wakirudi katika maeneo yao ya kazi wataweza kuwatambua wafanyakazi wanaopata magonjwa au ajali zitokanazo na kazi na wataweza kufidiwa na WCF hivyo kuweza kurudi katika kazi za ujenzi wa taifa.



