Madereva bajaji, bodaboda wafundwa madhara dawa za kulevya

ARUSHA: Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafirishaji Ardhini (LATRA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa elimu juu ya madhara ya usafirishaji haramu wa dawa za kulevya na kemikali bashirifu kwa madereva bodaboda na bajaji zaidi ya 200 wa Wilaya ya Arusha.

Madereva hao wa bajaji na bodaboda wameahidi watakuwa mabalozi wa kupinga  dawa za kulevya na kufikisha elimu juu ya madhara ya tatizo la dawa za kulevya kwa madereva wenzao kwa ujumla

Akizungumza na madereva hao wakati akitoa mada katika kikao cha usafirishaji kilichofanyika jijini Arusha ,Ofisa wa Mafunzo na Elimu wa Mamlaka DCEA, Shabani Miraji amesema tukio hilo ni endelevu kuhakikisha matumizi ya dawa za kulevya nchini yanapigwa vita kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali.

Advertisement

Amesema  wasafirishaji hao ni sehemu muhimu ndio maana wamekuwa kutoa elimu hiyo ili  kuhakikisha vita dhidi ya dawa za kulevya nchini inakuwa historia .

Awali akiongea mara baada ya kikao hicho Ofisa udhibiti wa Kemikali bashirifu kanda ya kaskazini ,Thomas Muhesa amesema lengo la  kukutana na kundi kubwa ambao wanatoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo mbalimbali kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

“nyie ni  kundi na mnasafirisha mizigo bila kujua unachotumwa ni kitu gani na ni wahanga wakubwa  kwa maana kwamba wanasafirisha dawa za kulevya  kama bangi mirungi na heroine lakini pia wanaweza kusafirisha kemikali bashirifu ambazo zinatengeneza dawa za kulevya”

Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Maofisa usafirishaji (bodaboda) Hakim Msemo amesema elimu hiyo waliyopewa itawasaidia  kutokomeza dawa hizo kwa sababu dawa za kulevya zimekuwa ni tatizo ndani ya nchi na yanauzwa mitaani huku vijana wanayatumia na kuharibikiwa kimaisha.