Madereva wazembe kuchukuliwa hatua za kisheria

JESHI la Polisi itaendelea kuchukua hatua za kisheria kwa madereva wazembe na wasiozingatia sheria za usalama barabarani na kuwasababishia maafa watu wengine.
Kamishna wa Polisi wa Operesheni na Mafunzo (CP), Awadhi Juma Haji amesema hayo leo alipowatembelea majeruhi wa ajali waliolazwa wodi za mifupa na wodi za upasuaji kwenye hosipitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro akiwa kwenye ukaguzi wa ajali ya magari mawili yaliyogongana majira usiku wa Desemba 17, 2024.
Watu 15 wamepoteza maisha na wengine saba kujeruhiwa kutokana na ajali ya gari ndogo ya abiria aina ya Toyota Coaster kugongana uso kwa uso na gari kubwa la mizigo katika kijiji cha Benderaa mbili ,Kata ya Mikese , Wilaya ya Morogoro katika Barabara Kuu ya Morogoro- Dar es Salaam.
Kamishna wa Jeshi hilo aliambatana na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Naibu Kamishna Ramadhani Ng’anzi, pamoja mwenyeji wao Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Alex Mkama.
“Nimekuja kuona tukio hili la ajali mbaya iliyoleta maafa haya makubwa ambayo yametokea kutokana na uzembe wa dereva wa Lori na kuwaona mliopata majereha na kulazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro,” amesema Haji akiwa kwenye wodi za majeruhi hao .
Kwa mijibu wa Kamishna wa Jeshi hilo kuwa ajali hiyo ilihusisha magari mawili moja ni Basi dogo aina ya Toyota Coaster ambayo ikitokea mjini Morogoro kuelekea Dar -es-Salaam pamoja na gari kubwa la mizigo lenye namba za usajili T715 DZX likitokea upande wa Dar es Salaam kuelekea Morogoro
Kamishina wa Jeshi hilo amesema katika ajali hiyo watu 14 walifariki dunia papo hapo na kati ya hao 14 ,wawili ni madereva wa Basi dogo Coaster pamoja na wa gari hilo kubwa la mizigo.
Amesema chanzo cha ajali hiyo kinaonesha kwamba ni uzembe wa dereva wa gari Lori ambaye alikuwa akitokea upande wa Dar es Salaam kuelekea Morogoro.
Amesema kuwa alipofika katika eneo hilo hakuwa makini ,hakuwa na tahadhari zozote na alianza kuyapita magari ya mbele yake bila kuzingatia watumiaji wengine wa barabara.
“Chanzo kikubwa ni uzembe wa huyu dereva wa Lori ambaye alikuwa akiyapita magari yaliyombele yake bila kuchukua tahadhari ,lakini eneo hili pia ni lenye kona na dereva alipaswa azingatie hilo,” amesema.



