MADIWANI na viongozi mbalimbali katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara watahakikisha wanasimama imara kuona watoto wao hawaathiriki na mchezo wa kamali (maarufu Dubu).
Akizungumza wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo ya Tandahimba, Diwani wa Kata ya Nanyanga kwenye halmashauri hiyo, Abasi Shaibu amesema wanalo wimbi kubwa la wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari ambao kwa sehemu kubwa wamekuwa washiriki mchezo huo hasa kipindi hiki cha msimu wa korosho mwaka 2024/2025.
Kikao hicho kimefanyika leo Novemba 14, 2024 kwenye halmashauri hiyo, kuhusu kupitia taarifa za miradi mbalimbali ya maendeleo kutoka kwenye kata mbalimbali robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
“Madubu haya yamekuwa yakisimamiwa na wafanyabiashara ambao ni wachina wamekuwa wakisambaza kwenye vijiji vingi na maeneo mengi kwenye halmashauri hii mfano mimi kwenye kata yangu ya Nanyanga hayo madubu hayakosi kuwa 7 mpaka 8″amesema Abasi.
“Na sisi kama viongozi tunaendelea kupambana na kusimamia kuona kwamba madubu hayaathiri vijana hasa watoto wetu kwasababu ni changamoto ambayo inaathiri watoto wengi kwahiyo tutahakikisha haya madubu na mabonanza yanatakiwa kuchezwa na watu wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea”
Diwani wa Kata ya Namikupa kwenye halmashauri hiyo, Mohamedi Ibrahimu amesema kutoka na uwepo wa changamoto hiyo ipo haja ya kuipatia ufumbuzi kwakuwa athari wanayoipata katika usimamizi na malezi ya jamii yao ni tofauti na faida ambayo serikali inapata.
“Serikali inatuhimiza wazazi, walezi kuwasimamia watoto kwa kushirikia na wataalam wao kuwapeka watoto shule mwisho wa siku watoto hao wakishaenda kusoma shule wakirudi kitu cha kwanza ni kwenye bonanza, sasa alichokisoma shuleni akifika pale kinayeyuka na kuanza kuwaza kamali”
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Baisa Abdala amesema halmashauri itabidi iandae sheria ndogo ya kuzuia vitendo hivyo vya kubashiri kwa watoto chini ya umri huo wa miaka 18 na kwa yeyote atakae kiuka atafunguliwa mashtaka.
Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Michael Mntenjele amesema kama kuna mtu anachezesha mchezo huo kwa watoto wadogo siyo sahihi kwani uchezwe kaunzia umri huo wa miaka 18.
“Lazima kama kuna watu wanachezesha mchezo huo kwa watoto chini ya umri wa miaka 18 waelimishwe kwasababu siyo sahihi kucheza watoto wadogo, mfano hawa watoto wa sekondari akishajua kuna kula pale kidogo anatafuta hela matokeo yake anajihusisha na vitendo vya wizi”amesema Mntenjele