MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Grace Quintine amefunga mafunzo ya kuhuisha mpango mkakati wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo yaliyolenga kuboresha ufanisi wa kiutendaji wa halmashauri.
Mafunzo hayo yametamatika jana ambapo yalianza Desemba 16 na kuhusisha Wakuu wa Divisheni na Vitengo vya Halmashauri ya Wilaya ya Urambo.
Akizungumza katika tukio la kufunga mafunzo hayo, Quintine amesema amefurahishwa na utulivu na uwezo mkubwa wa wakuu wa Divisheni na Vitengo wa kusikiliza na kufuata maelekezo ya wakufunzi, ambapo kupitia mpango mkakati uliohuishwa halmashauri itanufaika.
Ameendelea kusema kuwa, faida ya kuwa na mpango mkakati ni kusaidia kuongeza ufanisi na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea ili kuendana na kasi na sera za kitaifa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan pamoja na sera nyingine za kanda, bara na dunia.
Ikumbukwe kuwa Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kupitia ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji iliandaa mafunzo ya Siku tano (05) kwa Wakuu wa Divisheni na Vitengo yaliyoratibiwa na wakufunzi kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo – Dodoma ili kuhakikisha inahuisha Mpango mkakati wake.
Mafunzo hayo mpaka sasa yametoa matokeo chanya ambapo kwa hatua za awali Mipango na Vipaumbele vya kila Divisheni na Kitengo cha Halmashauri vimewekwa, hivyo basi kukamilika kwa mpango mkakati huu kutaleta mabadiliko katika utendaji na kuongeza ufanisi.
“Ninatarajia kila mmoja wetu atakamilisha mpango wa Divisheni/Kitengo kwa kushirikiana na watumishi waliopo chini yake ili tuweze kuandaa mpango wa pamoja utakaowezesha Halmashauri yetu kuwa na Dira na muelekeo wa kiutendaji ndani ya muda tuliojiwekea” Quintine amesema