Mahakama itekeleze aliyoagiza Samia kufanikisha Dira 2050

JANA Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza Mahakama ya Tanzania itekeleze mambo 12 kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050.

Rais Samia aliyasema hayo kupitia hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Rais, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria na uzinduzi wa Mwaka Mpya wa shughuli za kimahakama wa 2026.

Alisema mahakama ina wajibu muhimu wa kulinda utawala wa sheria, kusimamia utekelezaji wa mikataba, kulinda rasilimali za taifa na kuhakikisha maendeleo yanayopatikana yanawanufaisha Watanzania wote kwa usawa.

Alisema Mahakama ina mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050, hivyo iendelee kulinda haki na misingi ya Katiba na kuhakikisha migogoro ya kiuchumi, kibiashara na kijamii inatatuliwa kwa haraka na kwa haki.

Aliagiza Mahakama kujenga imani ya wananchi na wawekezaji katika mfumo wa kisheria wa nchi na kukuza uwajibikaji na nidhamu katika utumishi wa umma na sekta binafsi.

Aliitaka kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa ambao ni msingi wa maendeleo endelevu na kuwezesha mazingira bora ya uwekezaji na ukuaji wa uchumi kwa kuhakikisha utawala wa sheria unazingatiwa.

Rais Samia alisema Mahakama ina wajibu wa kulinda haki za makundi maalumu wakiwemo wanawake, watoto na watu wenye mahitaji maalumu, hivyo izuie migogoro inayoweza kuwa chanzo cha migawanyiko ya kijamii au kisiasa.

Aidha, aliitaka kuharakisha utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo kwa kutoa tafsiri ya kisheria iliyo wazi na thabiti, kujenga na kuimarisha utamaduni wa kuheshimu sheria, haki na taasisi za umma.

Eneo jingine aliloagiza ni mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka kwa kutoa haki bila upendeleo.

Maagizo hayo ya Rais Samia pamoja na hili la kuwataka majaji na mahakimu wasitumie uhuru wa mahakama kama kichaka cha kuficha uzembe, upendeleo au vitendo visivyo vya haki, yanaakisi taswira chanya ya utekelezaji wa Dira 2050.

Tunaungana na Rais Samia kuhimiza Mahakama na watendaji kuzingatia maagizo haya ili mahakama iendelee kuwa mahali salama pa wananchi kukimbilia kupata haki ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dira hiyo.

Tunakazia maagizo ya Rais Samia kwamba kamwe uhuru wa mahakama usitumike kama kichaka cha kuficha uzembe na kusisitiza haki kama alivyoahidi Jaji Mkuu, George Masaju kwamba chombo hicho kitaisimamia.

Katika utekelezaji wa dira hii kama alivyoagiza Rais Samia, tunaikumbusha mahakama si tu iwe chombo cha mwisho cha utoaji haki nchini, bali iwe mshirika muhimu katika safari ya maendeleo ya taifa.

Habari Zifananazo

2 Comments

  1. I get paid more than $120 to $130 per hour for working online. I heard about this job 3 months ago and after joining this i have earned easily $15k from this without having online working skills.
    This is what I do…..  www.join.work27.com

  2. I get paid more than $120 to $130 per hour for working online. I heard about this job 3 months ago and after joining this i have earned easily $15k from this without having online working skills.
    This is what I do….. …………………………………………………………………………….. www.join.work27.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button