Mahakama kutoa uamuzi kesi ya Lissu Jumatatu

DAR ES SALAAM; MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam Jumatatu ijayo inatarajiwa kutoa uamuzi wa kesi ya kusambaza taarifa za uongo inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.

Uamuzi huo utatolewa baada ya upande wa mashitaka kujibu mapingamizi yalizowasilishwa na mawakili wa utetezi juu ya utaratibu wa kesi hiyo kusikilizwa kwa njia ya mtandao na si kuletwa mahakamani.

Pia, pamoja na changamoto za kimtandao zilizojitokea wakati wa kusikiliza kesi hiyo Lissu aligoma kuendelea na kesi kwa njia ya mtandao.

Mwanasiasa huyo yupo katika gereza la Ukonga wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Kesi hiyo ilianza kusikikizwa saa 3:15 asubuhi mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini wakati ilipotajwa kwa ajili ya kusomwa hoja za awali kwa njia ya mtandao mahakamani hapo.

Ilidaiwa aligoma baada ya kupelekewa taarifa na Askari Magereza akiwa mahabusu kwamba anatakiwa afike katika chumba cha video cha gereza hilo kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa kesi yake, yeye aligoma na kudai hawezi kusikiliza kwa video.

Awali, wahusika wa masuala ya Tehama mahakamani hapo walihangaika kwa muda kuunganisha katika mtandao mawakili wa serikali, Gereza la Ukonga alipo Lissu na upande wa mahakama alipokuwa hakimu na mawakili wa utetezi ili waweze kusomana.

Wakati hali hiyo ikiendelea kwa dakika kadhaa hakimu alisitisha kesi hiyo hadi pale atakapopata uthibitisho kutoka magereza kama Lissu yupo wakati akiendelea kusomana na mawakili wa serikali kuhakikisha wanamsikia kwa sababu hawakuwapo mahakamani pia.

Ilipofika saa 3:24 asubuhi Hakimu Mhini alianza kwa kuita tena ili apate uthibitisho kama Lissu yupo mahakamani na pia kama mawakili wa serikali wanamsikia, askari wa Jeshi la Magereza aliyeonekana kutoka Ukonga alimuomba hakimu kama dakika mbili wamlete, kwa hiyo aliomba mahakama ivumilie kidogo.

Katika kesi hiyo Lissu anatetewa na zaidi ya mawakili 25 na wakati hali hiyo ikiendelea moja ya mawakili hao, Mpare Mpoki alimueleza hakimu kwamba wanapoteza muda na kueleza kuwa vitabu vipo na vinaweza kutumika yaani Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Hakimu Mhini alimjibu kuwa hawezi kuendelea hadi apate uthibitisho wa hali ya mtandao kutoka pande zote mbili na ilipofika saa 3:59 asubuhi Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga aliieleza mahakama kuwa wapo tayari kuendelea.

Baada ya mtandao kuwa sawa askari magereza aliyepeleka taarifa ya Lissu kufikishwa katika chumba cha video kwa ajili ya kesi alidai kuwa walipomfikishia taarifa Lissu alidai hawezi kuendelea na kesi kwa njia ya mtandao.

Kesi hiyo iliendelea kusikilizwa pamoja ya kuwa mshitakiwa aligoma kuendelea kusikiliza kwa njia ya mtandao na wakati ikiendelea mawakili wake wa utetezi wakiongozwa na Mpoki aliyeungana na Peter Kibatala na Jeremiah Ntobesya waliwasilisha pingamizi zao mahakamani hapo.

Miongoni mwa hoja zao za mapingamizi ni kwamba wanapinga utaratibu wa kesi hiyo kusikilizwa kwa njia ya mtandao huku wakitaka mtuhumiwa afikishwe mahakamani kwani ili asomewe maelezo ya awali (Ph) lazima upande wa Jamhuri, Utetezi na Mtuhumiwa wawepo mahakamani sambamba na mtuhumiwa kusaini karatasi ya maelezo.

“Hata kama mtuhumiwa angekuwepo mtandaoni leo tusingeweza kuendelea kwa sababu ingekuwa ni kinyume na sheria kwa sababu sheria inataka maelezo ya awali yafanyike mtuhumiwa akiwepo,” alisema Mpoki.

Baada ya kuelezwa hayo hakimu ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 28, 2025 kwa ajili ya kutoa uamuzi wa mapingamizi hayo ya utete kwa njia ya mtandao ili kuona kama kesi hiyo isikilizwe kwa mtandao ama mshitakiwa afikishwe mahakamani.

Katika kesi hiyo ilidaiwa Aprili 3, 2025 katika shitaka la kwanza Lissu alichapisha taarifa inayosema, “Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 wagombea wa Chadema walienguliwa kwa maelekezo ya Rais,” wakati akijua si kweli.

Katika shitaka la pili inadaiwa Aprili 3, 2025 Lissu kupitia mtandao wa Youtube alichapisha taarifa inayosema ‘Mapolisi wanatumika kuiba kura wakiwa na vibegi’ wakati akijua si kweli.

Na shitaka la tatu alidai Lissu alichapisha taarifa ya uongo kwa nia ya kupotosha umma kupitia mtandao wa youtube inayosema: “Majaji ni ma-CCM hawawezi kutenda haki wapate teuzi na kuchaguliwa kuwa majaji wa mahakama ya rufaa” wakati akijua tarifa hiyo ni uongo na inapotosha umma.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button