Mahakama yatoa mwaka marekebisho kesi ya kiraia

MAHAKAMA ya Rufaa ya Tanzania jana imetoa uamuzi wa Rufaa Na.134 ya Mwaka 2022 ya kesi ya Kikatiba iliyokuwa inapinga vikwazo katika ufunguaji wa mashauri yenye maslahi kwa umma ambapo imetoa muda wa Miezi 12 kwa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya marekebisho.
Vifungu vilivyoainishwa kufanyiwa marekebisho ni vifungu namba 4(2),4(3),4(4) na 4(5) vya Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu vilivyotungwa kupitia Sheria ya Mabadiliko ya sheria Mbalimbali (Na.3) ya Mwaka 2020.
Kesi hiyo ilifunguliwa na Mtetezi Maarufu wa Haki za Binadamu Wakili Onesmo Olengurumwa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo rufaa hiyo ilisikilizwa na majaji watatu wa Mahakama ya rufaa ambao ni Jaji Levira, Jaji Rumanyika na Jaji Ngwembe.
Kwa upande wa Mrufani aliwakilishwa na Jopo la mawakili likiongozwa na Prof Issa Shivj, wakili mwandamizi Mpale Mpoki, Dk Rugemeleza Nshala na Wakili John Seka huku serikali ikiwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Hangi Chang’a na jopo lake.
Uamuzi wa rufaa hiyo umetolwa jana kwa njia ya mtandao na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa Mheshimiwa Joseph Fovo ambapo ameeleza kwamba Mahakama ya Rufaa imevibatilisha vifungu vya 4(2), 4(3), 4(4), na 4(5) vya Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu.
Akizungumza mara baada ya uamuzi huo Olengurumwa amesema mahakama imeamua kifungu cha 4(2) kinachoweka sharti la ulazima wa kuambatanisha kiapo kueleza namna mtu anayepeleka shauri Mahakama Kuu kuhusu ukiukwaji wa haki za kikatiba alivyoathirika binafsi linaondoa dhana au maana ya shauri la maslahi kwa umma hivyo kifungu hicho ni batili.
Amesema kwamba, kifungu cha 4(3) kinachoweka ulazima wa mtu anayetaka kufungua shauri lenye maslahi ya umma lazima aonyeshe maslahi binafsi kama inavyotakiwa kwenye Ibara ya 30(3) ya Katiba batili kwasababu Ibara ya 26(2) inayotoa haki ya kufungua shauri lenye maslahi kwa umma ni tofauti na Ibara ya 30(3) inayotaka maslahi binafsi.
“Kwamba kifungu cha 4(4) kinachoweka ulazima wa kumshitaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwaniaba ya Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika, Naibu Spika na Jaji Mkuu, ni batili kwasababu anamajukumu yake kikatiba na hahusiki kwa mfano na Jaji Mkuu hivyo hamna msingi wowote wa kisheria kuweka takwa hilo.
“Kifungu cha 4(5) kinachotaka mtu anayetaka kufungua kesi lazima kwanza atafute nafuu ya malalamiko yake kwenye sheria zingine zilizopo kabla ya kufungua kesi chini ya sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu ni batili kwasababu hakuna Sheria inayotoa nafuu hizo kwenye mashauri yenye maslahi kwa umma,”amesema.
Kwa Upande wake wakili wa Mrufani, Prof Shivji ameisifu mahakama wa rufaa kwa kutoa uoamuzi huo unaolenga maslahi ya wananchi wote.
“Nawapongeza jopo la majaji na mahakama kwa kutoa uamuzi lakini kwa ofisa mwandamizi kama mimi naweza kufanya hivyo kwasababu uamuzi huo umekuwa faraja kubwa nimewafundisha wanafunzi wengi mawakili na serikali na binafsi na majaji kwahiyo uamuzi kama huu unapotolewa inanipa faraja kubwa.
Ameongeza “Majaji wametoa uamuzi wenye ujasiri na mahakama ndio chombo cha mwisho kulinda haki za wananchi,haki ya kuishi ,sheria hizi zilikuwa zinaathiri wajibu wa kutetea umma.
Mnamo tarehe 19 Juni 2021, Serikali ya Tanzania ilichapisha katika Gazeti la Serikali Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) ya Mwaka 2020, iliyofanya mabadiliko makubwa katika Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu ambapo Olengurumwa alifungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania Februari 15,2022.
Hata hivyo Mahakama Kuu ilitupilia mbali kesi hiyo na kusema kuwa vifungu hivyo viko sawa na havipingani na Katiba wala mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu.



