Majaliwa aagiza mikakati kukomesha udumavu

DAR ES SALAAM : WAZIRI Mkuu , Kassim Majaliwa, ametoa maelekezo saba kwa wizara, taasisi za umma na wadau wa lishe nchini kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo maazimio yote ya kitaifa ikiwa ni jitihada za kupunguza udumavu na magonjwa yasiyoambukiza.

Alitoa maagizo hayo jana alipofunga mkutano wa 11 wa wadau wa lishe uliofanyika jijini Dar es Salaam.Amesema utekelezaji wa maazimio hayo utaongeza tija katika mapambano dhidi ya utapiamlo na kuboresha afya za Watanzania.

Miongoni mwa maelekezo hayo ni pamoja na kusambaza maafisa lishe waliopata mafunzo katika halmashauri zote, kuimarisha kamati za lishe kuanzia ngazi ya kata hadi vijiji, na kuimarisha ukaguzi wa vyakula vya nyongeza. SOMA: Wapewa mbinu kuepuka udumavu

Pia, taasisi za utafiti na vyuo vikuu vimetakiwa kuendeleza tafiti na kutumia matokeo yake kuboresha sera na mikakati ya lishe.Aidha, Waziri Mkuu ameagiza Wizara ya Fedha kuboresha mifumo ya ufuatiliaji ili kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya lishe zinatumika ipasavyo.

Wizara na taasisi mbalimbali pia zimetakiwa kutenga rasilimali za kutosha kwa afua za lishe na kuhakikisha mipango ya kila mwaka inazingatia uwajibikaji na uendelevu. Alisisitiza pia umuhimu wa kuimarisha programu za utoaji chakula shuleni, elimu ya lishe kwa vijana na kulinganisha mikakati ya kilimo na mifumo ya chakula inayojali lishe bora.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, hatua zilizochukuliwa tayari zimechangia kupunguza kiwango cha udumavu wa watoto chini ya miaka mitano kutoka asilimia 48 mwaka 1992 hadi asilimia 30 mwaka 2022. Hata hivyo, alionya kuwa changamoto mpya ni kuongezeka kwa tatizo la uzito kupita kiasi, hasa kwa wanawake ambapo kiwango kimepanda kutoka asilimia 28 mwaka 2015 hadi asilimia 37 mwaka 2022.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ridhiwani Kikwete, aliwashukuru wadau kwa ushirikiano na akibainisha kuwa Tanzania imefanikisha utafiti wa kitaifa wa utapiamlo ambao matokeo yake yatatumika kama nyenzo muhimu ya kutunga sera. Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Jimmy Yonazi, alisema wadau 340 walioshiriki mkutano huo wamekubaliana kuimarisha ubunifu katika upatikanaji wa fedha, matumizi ya teknolojia na ushiriki wa jamii katika mapambano dhidi ya udumavu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button