WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametembelea banda la Mamlaka ya Serikali Mtandao(e-GA) na kujionea shughuli mbalimbali ikiwemo mfumo shirikishi wa kusimamia shughuli za rasilimali za taasisi ujulikanao kama Enterprise Resource Management System’ (ERMS).
Akizungumza katika banda hilo leo Novemba 4, 2024 wakati wa mkutano wa tisa wa Mtandao wa Mameneja na Wasimamizi wa Rasilimali Watu katika Sekta ya Umma Afrika (APS-HRMnet) unaofanyika Arusha kwa siku nne, Majaliwa ameupongeza mfumo huo kwa kuimarika.
Akifafanua kuhusu namna unavyofanya kazi mfumo huo, Ofisa Habari Mwandamizi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Queenter Mawinda mbele ya Waziri Mkuu amesema mfumo huo umesaidia kuimarisha utendaji kazi wa taasisi kupitia moduli 20 zinazounganisha shughuli za idara na vitengo.
Amesema kupitia mfumo huu ufanisi wa kazi wa vitengo na idara umeongezeka lakini pia kuboresha usimamizi mzuri wa rasilimali za taasisi.
“Mfumo wa ERMS umeboresha utoaji wa huduma kwa kuunganisha shughuli za Idara na Vitengo ndani ya Taasisi kupitia module zinazopatikana ndani ya mfumo huo,”
Ametoa rai kwa taasisi ambazo bado hazijajiunga na mfumo wa ERMS kufanya hivyo mapema ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa Taasisi zao kwa ajili ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi.