Majaliwa akiri Ndugai amemsaidia majukumu bungeni

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Spika mstaafu wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai alikuwa msaada mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yake bungeni.

Majaliwa alisema hayo wakati wa ibada ya kuaga mwili wa Ndugai katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma jana.

Alisema alipokuwa Naibu Waziri na Waziri Mkuu, Ndugai alimsadia katika utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kiserikali bungeni ikiwemo miswada na sheria.

“Nimefanya nae kazi ndani ya Bunge toka mimi nikiwa Naibu Waziri na yeye akiwa naibu spika na baadaye kwa nafasi niliyonayo na yeye akiwa spika kamili nilipata ushirikiano wa dhati katika kutekeleza majukumu yangu ndani ya Bunge,” alisema Majaliwa.

Alisema kutokana na ushirikiano huo aliweza kutekeleza majukumu kwa weledi wa hali ya juu na kubainisha kuwa Hayati Ndugai anapaswa kukumbukwa kwa mambo mengi ambayo ameifanyia nchi wakati wa uhai wake.

“Tunayo majukumu makubwa mawili moja kuyaenzi yale yote mazuri aliyotekeleza wakati wa uhai wake, utumishi wake na kuendeleza yale aliyopanga ili yaweze kutimia,” alisema.

Majaliwa alitoa pole kwa Rais Samia, Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson, familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa kifo cha Ndugai.

“Tumepokea taarifa ghafla imetuumiza lakini yote ni kazi yake Mwenyezi Mungu kwa niaba ya wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Mazishi ya Viongozi wa Serikali pamoja na mwenyekiti mwenza Makamu wa Pili Zanzibar mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla tunamuombea alale mahali pema peponi,” alisema.

Kwa upande wake Abdulla alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inathamini mchango wa Ndugai alioutoa kwa SMZ wakati wa uhai wake.

Alisema Ndugai akiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa mstari wa mbele kutoa ushauri na ushirikianao kwa serikali hiyo.

“Kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Wanzanzibari wote tunapenda kutoa pole tena kwako mheshimiwa Rais, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na familia ya marehemu na Watanzania wote na tunaomba Mungu ailaze roho ya marehemu pema peponi,” alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button