Majaliwa asema teknolojia mpya si tishio, bali fursa

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amevitaka vyama vya wafanyakazi Afrika kuweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia duniani.

Aidha, aliainisha mikakati minne ambayo serikali ya Tanzania imejizatiti kukabiliana na mabadiliko hayo.

Ameyasema hayo Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Afrika (OATUU) alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Alisema ingawa nguvu hizo za mabadiliko zinafanya fursa mpya za uvumbuzi, uzalishaji na ukuaji lakini zinaleta wasiwasi mkubwa kwani kuna hatari ya watu kupoteza ajira wakati mashine na mifumo inapoanza kutekeleza majukumu waliyokuwa wakifanya wafanyakazi.

“Mbali na hayo kuna kupungua kwa kipato, ukosefu wa ulinzi wa haki za kazi na pia kumekuwa hakuna faragha na uhuru kwa ujumla,” alisema.

Alisema kama vyama vya wafanyakazi vitaweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko hayo ya teknolojia, kutapunguza hatari ya watu kupoteza ajira kutokana na ujio wa mashine na matumizi ya teknolojia mpya ikiwemo ya akili mnemba.

“Hakuna asiyeathirika na nguvu hizi za kimataifa, hivyo mageuzi na kujitolea kwa pamoja ni muhimu kwa siku zijazo… kwa kutambua hili, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, serikali yetu imejizatiti si tu kukabiliana na mabadiliko haya, bali pia kuyatumia kwa manufaa ya watu wetu,” alisema.

Akiitaja mikakati hiyo, Majaliwa alisema ni kuzidisha ulinzi wa kijamii na mageuzi ya mifumo ya usalama wa kijamii ili kuhakikisha inawalenga si tu wafanyakazi wa sekta rasmi, bali pia mamilioni walio katika uchumi usio rasmi, kuimarisha na kujifunza kufanya uwekezaji mkubwa katika programu za mafunzo na kuongeza ujuzi.

Alisema mkakati mwingine wa Tanzania ni kuhamasisha matumizi yanayohusika ya teknolojia, ikiwemo akili mnemba huku ikiweka tahadhari ya kulinda haki za wafanyakazi na faragha.

Aliongeza: “Teknolojia inapaswa kuhudumia ubinadamu, haipaswi kudhoofisha heshima ya kazi. Zaidi ya yote Tanzania inaendelea kujitoa kulinda misingi ya kazi nzuri na haki za kijamii kwa wote. Kwa Tanzania, maisha ya kazi hayapaswi kufafanuliwa kwa unyanyasaji au kutengwa bali kwa usawa, fursa na haki kwa kila mfanyakazi”.

Alisema serikali inathamini na kutambua mchango mkubwa wa vyama vya wafanyakazi nchini na itaendelea kushirikiana nao katika kuboresha masilahi ya wafanyakazi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi alisema serikali imeendelea kushirikiana na vyama vya wafanyakazi nchini na imepitisha sera na sheria mbalimbali katika kuhakikisha inarekebisha na kuboresha masilahi ya wafanyakazi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button