Majaliwa: Wavuvi ruksa kuuza samaki popote

GEITA; WAZIRI Mkuu, Kassimu Majaliwa, amesema wavuvi wa samaki na dagaa wanaruhusiwa kuuza kwenye mwalo ama soko lolote nchini na hakuna halmashauri itazuia.

Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza na wavuvi na wafanyabiashara wa samaki na dagaa, mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika soko la kisasa la mazao ya samaki mwalo wa Chato.

Amesema uamuzi huo umekuja kufuatia baadhi ya halmashauri ikiwemo Chato (Mganza) na Mleba kuripotiwa kuwa na mvutano kugombania wavuvi, hali iliyoathiri maendeleo ya shughuli za uvuvi.

“Tumewaambia hakuna kuwazuia wavuvi kuuza samaki popote, mvuvi anayo fursa ya kupeleka samaki popote, hata kama bahari (ziwani) ipo kandokando yako,” amesema.

Amesema serikali imejizatiti kuboresha mialo yote nchini, ili kukuza sekta ya uvuvi kupitia ujenzi wa maeneo ya kisasa ya kuhifadhi na kuuza samaki kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.

Amewaomba Watanzania kuchangamkia fursa ya uvuvi, ambapo wanaweza kuanzisha vikundi kwa ajili ya kunufaika na mpango wa uwezeshaji kiuchumi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na halmashauri.

Amesema tayari ofisi yake imekuja na mpango wa kuikusanya na kuiweka pamoja mifuko yote inayotoa mikopo, ili iwe rahisi kwa wananchi kuifikia.

Ameelekeza ofisi ya mkurugenziwa halmashauri kusimamia uundaji vikundi na utoaji elimu kwa wavuvi, ili waweze kukopesheka na kuendesha shughuli zao kibiashara zaidi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Mandia Kihiyo amesema mradi wa mwalo wa kisasa umegharimu Sh bilioni 1.7 na utanufaisha wafanyabishara wa samaki wapatao 1,120.

Habari Zifananazo

Back to top button