Maji muhimu kwa uchumi wa nchi-Mkuchika

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Kazi Maalum, George Mkuchika amesema kuwa upatikanaji wa maji safi na salama nchini ni muhimu kwa maendeleo ya watu ili kuwezesha muda mwingi kutumika kwa shughuli za maendeleo badala kutafuta maji.

Waziri Mkuchika amesema hayo alipotembelea na kukagua mradi mkubwa wa maji katika mji wa Buhigwe ambapo alipata nafasi ya kuzungumza na wananchi baada ya kukagua mradi huo ikiwa ni ziara za kuzungumzia mafanikio ya serikali ya awamu ya nne.

Amesema serikali ina miradi mingi ya kiuchumi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na biashara kwa wananchi hivyo muda mwingi unahitajika kwa wananchi kushiriki shughuli za uchumi badala ya kuhangaika kutafuta maji ndiyo maana serikali imeweka mkazo kuhakikisha maji safi na salama yanapatikana umbali mfupi kutoka wanapoishi wananchi.

Amesema kuwa serikali inatekeleza miradi kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo inataka maji safi na salama yapatikane vijijini kwa asilimi 85 na mijini kwa asilimia 95 na kazi kubwa imefanyika kuhakikisha maji safi  na salama yanapatikana nchi nzima ambayo imewekwa kwenye dira ya taifa 2020 hadi 2025.

Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuchika, Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Buhigwe, Golden Katoto amesema kuwa mradi huo utakapokamilika watu 66,406 kutoka vijiji vinane vya Buhigwe watanufaika na upatikanaji wa maji safi na salama na kwamba mradi huo unatarajia kukamilika mwezi Juni mwaka huu.

Katoto amesema kuwa mradi huo unatarajia kugharimu kiasi cha Sh bilioni 9.7 ambapo kati ya hizo kiasi cha Sh bilioni 5.06 zinatoka Benki ya aendeleo ya Afrika (AFDB) ikiwe ni sehemu ya kusaidia shughuli za kijamii katika mradi mkubwa wa barabara ya Kiwango cha lami kutoka Manyovu wilaya ya Buhigwe hadi Kabingo wilaya ya Kakonko kilometa 260.6.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button