Makonda asema Miradi ya CCM inaacha alama

ARUSHA : MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Paul Makonda ametaja miradi iliyotekelezwa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaacha alama. Makonda alisema hayo katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha wakati wa mkutano wa kampeni za mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan.
“Uaminifu wako na maelekezo uliyonituma katika mkoa huu na hatimaye kila wilaya, kuna alama ya kazi ya mikono yako mgombea wetu wa urais, Samia Suluhu Hassan,” alisema. Alieleza miradi iliyoacha alama ya Rais Samia ni upanuzi wa Kiwanja cha Ndege Arusha cha Kisongo na kusaidia ndege ndogo zinazofanya safari zake kila siku kutoka Arusha hadi Nairobi, kwa ajili ya kuongeza idadi ya watalii.
“Umefanya kazi iliyokwama kwa miaka mingi. Kwa maelekezo yako, ndani ya mwaka huu tunayo miradi yenye thamani ya Shilingi bilioni 64 na sasa inatekelezwa Arusha Mjini. Tulikuwa na changamoto ya mabasi ya stendi lakini sasa inajengwa pamoja na ujenzi wa soko kubwa,” alisema.
Alisema kulikuwa na changamoto ya umeme, ambayo Rais Samia alielekeza wananchi wapatiwe umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ambapo wananchi wanaendelea kuunganishwa kwa Sh 27,000 pamoja na utatuzi wa changamoto za sekta ya afya na miundombinu ya elimu. SOMA: Mfumo wa stakabadhi ghalani utasimamiwa
Makonda alimuomba mgombea huyo akichaguliwa kuwa rais kufanya ujenzi barabara ya kwenda Sokoni Wani, Mulieti, Taleti, Mushono, Sakina, Balaha na Barabara ya Noracity. Alimuomba mgombea huyo atakapoingia madarakani, aikumbuke Arusha ya viwanda kwa sababu vijana wa jimbo hilo ni wachapakazi, hivyo alimsisitiza kufufua viwanda ikiwemo cha matairi. Pia, alimshukuru Samia kwa kumuamini kumteua kushika nafasi mbalimbali ikiwemo Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi. Kitendo hicho kimeonesha kiongozi huyo anawaamini na kuwalea vijana.



