DAR ES SALAAM: MBUNIFU wa mavazi nchini, Malika Rashid ‘Malika Designer’ amesema katika harakati zake za kusaidia jamii kwa kutoa misaada mbalimbali, Serikali imekuwa ikimuunga mkono kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza na mtandao wa HabariLEO mapema leo, Malika ameeleza kuwa baadhi ya viongozi au taasisi za serikali zimekuwa zikimuunga mkono sana kwenye suala la kuhudumia jamii na kumfanya kuendelea na harakati hizo akiamini serikali haiwezi kufanya kila kitu kwani wanapaswa pia kuisaidia.
“Niliwahi kumchangishia mtoto mmoja alikuwa na miaka tisa, nakumbuka nilimposti kwenye Instagram yangu, nakumbuka palepale CCBRT walinipigia simu wakasema mlete huyo mtoto, pia nilichangisha Sh milioni 12 kwa simu tano, pia kipindi kile Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate naye alingangia,” amesema Malika.
Malika amesema katika harakati zake anatamani kusaidia zaidi watoto akiamini ndio taifa la kesho.
“Lengo langu ni kusaidia watoto na wazee, Mungu aniwezeshe niweze kufanya hilo, kwasababu watoto wanapata shida sana,”amesema Malika.