Malipo kieletroniki kupunguzwa kodi

KIGOMA: MAMLAKA ya Mapato (TRA) imesema wananchi watakaofanya manunuzi ya bidhaa kwa njia za kielektroniki ikiwemo benki na mitandao ya simu watafaidika kwa kupata punguzo la kodi la bidhaa wanazonunua.
Ofisa Msimamizi Mkuu wa kodi TRA, Hamad Mterry alisema hayo katika mkutano na wafanyabiashara, wakuu wa mamlaka za serikali, vyombo vya ulinzi na usalama na wadau mbalimbali wa biashara na kodi mkoa Kigoma wakati akitoa elimu ya mabadiliko ya sheria ya fedha ya mwaka 2025.
Mterry alisema kuwa katika mabadiliko hayo ya sheria ya fedha ya mwaka 2025 wananchi hao watapata punguzo la kodi ya ongezeko la thamani kwa kulipa asilimia 16 badala ya 18 na kwamba hiyo inachochea wananchi kufanya malipo kwa njia za kielektroniki badala ya kutembea na pesa taslimu.
Pamoja na punguzo hilo alisema kuwa mabadiliko ya sheria ya fedha yanayofanyika kila mwaka yamekuwa na mchango mkubwa katika kuifanya mamlaka hiyo kuongeza ukusanyaji mapato na wakati mwingine kuwezesha kuvuka lengo.
Mmoja wa washiriki wa Mkutano huo, Celestine Nestory kutoka chemba ya wafanyabiashara, wenye viwanda na kilimo (TCCIA) Mkoa Kigoma alisema kuwa mkutano huo umekuwa na mafanikio makubwa kwao kujua manufaa ya mabadiliko hayo ya sheria ya fedha kwa wafanyabiashara, mamlakaa za usimamizi za serikali na mlolongo mzima wa kuweza kulipa kodi kwa hiari.