Mamakafa; mmea wenye maajabu kukwepa maadui

TANZANIA ni miongoni mwa mataifa duniani yenye utajiri mkubwa wa mimea ya aina mbalimbali ikiongozwa na ile ya asili.

Mimea hiyo inatumiwa na wengi kwa namna na manufaa mbalimbali kwani ipo inayotumiwa kama chakula ikiwamo ya matunda, mboga za majani na mizizi kama mihogo na viazi.

Vyanzo vinasema mimea hiyo pia ipo inayotumika kama kuni na mingine ikitumika kama tiba (dawa) na katika ulimwengu huu wa mimea, ipo mingi inayovutia kutokana na maumbo, harufu, rangi au tabia.

Kati ya mimea hiyo, upo mmoja unaoshangaza wengi kutokana na tabia yake ya kipekee ya kujibu au kuitikia mguso wa nje na pia, una tabia ya ajabu na ya kuvutia kwa namna unavyoweza kujilinda huku ukiwa hauna akili wala viungo vya fahamu.

Mmea huo unaojulikana kwa jina la ‘mamakafa’, kisayansi hujulikana kama ‘mimosa pudica’. Mamakafa ni moja ya maajabu ya ulimwengu wa mimea. Licha ya kuwa hauna akili wala misuli kama wanyama, mmea huo unaonesha uwezo mkubwa wa kujilinda na kuwasiliana na mazingira yake kwa njia ya pekee.

SOMA: Mpango ataka bustani kutafiti dawa

Tabia yake ya kujikunja unapoguswa si tu ya kuvutia, bali pia ni kielelezo cha namna uhai wa mimea ulivyo wa kushangaza na wa kuvutia zaidi kuliko wengi wanavyofikiria. Mmea wa mamakafa unafundisha kuwa, kila kiumbe katika asili yake kina mbinu zake za kuishi na kujilinda, hata kama hazionekani kwa ‘macho ya haraka’.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, jambo la kipekee zaidi kuhusu mamakafa ni tabia yake ya kujikunja au kunyauka kwa haraka jani lake linapoguswa, kutikiswa au likipata mabadiliko ya joto au mwanga.

Kitendo hiki cha haraka sana kwa mmea huo huitwa ‘thigmonasty’, yaani mwitikio wa mmea usioelekezwa, unaotokana na mguso. Chanzo kinasema: “Unapogusa mmea, hutokea mabadiliko ya haraka ya kemikali ambapo potassium iron (madini chuma ya potasiamu) hutoka nje ya seli na kusababisha maji kutoka.

“Seli hupoteza ‘turgor pressure’ (shinikizo la ndani) na jani hujikunja. Baada ya muda mfupi, maji hurudi katika seli na jani hurudi katika hali yake ya kawaida.” Kuhusu sababu za mamakafa kujilinda, vyanzo vinasema mwitikio huo si wa bahati mbaya wala wa mapambo ya asili.

“Mamakafa hutumia tabia hii kama njia ya kujilinda dhidi ya wanyama wanaokula majani. Majani yanapojikunja ghafla, huwatisha au kuwachanganya wanyama hao na hivyo mmea huendelea kuwa salama,” kinasema
chanzo mtandaoni.

Kinaongeza: “Mmea huu pia hujikunja wakati wa usiku. Tabia hii huitwa ‘nyctinasty’, jambo ambalo linadhaniwa kusaidia kuhifadhi maji au kuzuia uharibifu wa joto.”

Makala moja katika tovuti ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) iliyoandikwa Machi 21, 2018 na kuboreshwa Desemba 20, 2020 ikisema ‘Mimea Sita Yenye Sifa za Kushangaza Zaidi Duniani’ inautaja mmea wa aina ya mamakafa Vyanzo mbalimbali vikiwamo vya mtandaoni vinasema mamakafa ni mmea wenye majani ambayo ‘hujikunyata’ yanapoguswa.

BBC inasema: “Hii ni kutokana na kunyimwa maji na mmea wenyewe. Hii huaminika kuwa ni njia yake ya kujikinga dhidi ya wanyama wala nyasi na majani. “Wanyama wakubwa wanaweza pia kutiwa hofu na kujikunyata ghafla kwa majani hayo, wanaweza kuangushwa jani likijikunja,” inasema.

Katika ukurasa wa Facebook mtandaoni, Mandai Products Co. LTD inaandika chini ya kichwa cha habari: ‘Mamakafa Mmea wa Ajabu Unaofanya Maajabu katika Tiba’ ikisema nchini Tanzania, mamakafa hufahamika na watalaamu wa tiba kuwa ni mmea wenye maajabu huku nchi za ughaibuni wakiutambua kama mmea wenye hisia.

Andiko hilo linasema: “Unategemewa na matabibu wa tiba asili kufanyia mazindiko ya makazi ya wanadamu lakini pia kuganga magonjwa sugu yaliyoshindikana katika tiba za kisasa.” Desemba 29, 2021, Mtaalamu wa Virutubisho Tiba, Abdallah Mandai aliandika: “Yajue Maajabu ya Mamakafa Kitiba” akisema mamakafa ni mmea wenye maajabu makubwa katika tiba ya magonjwa mbalimbali.

Anasema: “…Pia, inaondoa mwasho sehemu za siri unaowakwaza kina baba na mama.” Mtaalamu mwingine, Amedi Abedi Novemba 15, 2020 aliandika kwenye ukurasa wake mtandaoni akisema mmea huu, “Hurudisha hisia za tendo la ndoa zilizotoweka kwa kina baba.”

Anaongeza: “Kausha majani yake kisha tumia katika uji usio mzito au katika maji moto.” Kimsingi, mmea huu unatajwa kuwa wenye faida lukuki kwa mwili wa binadamu ikiwa ni pamoja na kutumika kutibu kisukari, bawasiri, kuzuia kansa, kuondoa sumu mwilini na kutibu mtu aliyeng’atwa na nyoka.

Chapisho lililoandikwa mtandaoni na Taasisi ya Maintain YOUR Health chini ya Mtaalamu na Mshauri wa Sayansi ya Lishe Katika Matibabu, Dk Abdulatif linataja umuhimu wa mamakafa likisema upo pia katika matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwamo ya mifupa na maungio pamoja na magonjwa ya moyo na kurekebisha mapigo ya moyo.

Mbali na kuvutia kimtazamo, mamakafa hutumika pia katika tiba za jadi kwenye baadhi ya maeneo. Inaelezwa kuwa, mizizi na majani yake husaidia kutibu matatizo ya tumbo, majeraha ya ngozi na hata matatizo ya hedhi kwa wanawake.

Aidha, mmea huu hutumika kwa utafiti wa kisayansi, hasa katika kujifunza namna mimea inavyojibu vichocheo vya kimazingira. Inaelezwa kuwa, kwa kiasi kikubwa mmea huu si hatari kwa binadamu lakini haufai kuliwa kwa wingi na unaelezwa na vyanzo mbalimbali kuwa, unaweza kuwa sumu kwa baadhi ya wanyama kama mbuzi au ng’ombe endapo wataula kwa kiasi kikubwa.

Aidha, unatajwa kuwa muhimu kwa matumizi mengine yakiwamo ya utafiti wa kisayansi na hutumika katika maabara kufundishia wanafunzi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button