Mamalishe, babalishe Ubungo marufuku kupikia kuni, mkaa

DAR ES SALAAM; HALMASHAURI ya Manispaa ya Ubungo imetangaza marufuku ya kutumia kuni na mkaa kwa wananchi wote hasa wafanyabiashara wa chakula (baba na mamalishe) ifikapo Februari Mosi, mwaka huu.
Tangazo la marufuku hiyo lilitolewa Januari 14, mwaka huu likimnukuu Mkurugenzi wa Halmashauri akiwataka kuacha mara moja kutumia nishati hizo. Amesema endapo wataendelea na matumizi hayo hadi Februari Mosi, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
“Hivyo, kila mfanyabiashara anapaswa kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi, umeme, mkaa mbadala, bayogesi, ethano na nishati ya jua ili kulinda afya na kutunza mazingira,” lilieleza tangazo hilo.
Tangazo hilo lililosainiwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Joina Nzali, limeelekeza kwamba endapo mfanyabiashara atakutwa anatumia mkaa au kuni, hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kutozwa faini kuanzia Sh 50,000 hadi Sh 100,000 kutokana na Sheria ndogo za Manispaa na sheria mama ya mwaka 2004.
Tangazo hilo ni sehemu ya kuunga mkono utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 hadi 2034 ambao serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeuandaa ukilenga kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia kufikia asilimia 80 ya Watanzania watakaokuwa wanatumia nishati hiyo mwaka 2034.



