Mamalishe jela maisha kuishi kinyumba na mtoto
MTWARA: MAMALISHE Asha Chamchuno (46) amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la unyanyasaji wa kingono dhidi ya mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 15.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mtwara, Issa Suleiman alisema mamalishe huyo alikutwa akiishi kinyumba na mtoto huyo. Aliwaeleza waandishi wa habari kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Machi 22, mwaka huu.
Katika hatua nyingine Kamanda Suleiman alisema watu watatu wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 kwa kosa la kulawiti, kumpiga picha mwathirika wakati wakimlawiti, kurekodi video na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii. Aliwataja waliohukumiwa kuwa ni Shabibu Said aliyekuwa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na wezake watatu.
Alisema awali washtakiwa walihukumiwa kulipa faini ya Sh 1,000,000 katika Mahakama ya Wilaya ya Mtwara.
Kamanda Suleiman alisema baadaye upande wa Jamhuri ulikata rufaa katika Mahakama Kuu, Kanda ya Mtwara na rufaa hiyo ilisikilizwa Aprili 3, mwaka huu na Mahakama Kuu ilibatilisha adhabu na kuwa kifungo cha miaka 30 na washitakiwa wameanza kutumikia adhabu hiyo.