Mamia wamuaga Ndugai

MAMIA ya waombolezaji wameuaga mwili wa Mbunge wa Kongwa na Spika wa zamani wa Bunge, Job Ndugai (62) jijini Dodoma na Kongwa mkoani humo.
Awali, Rais Samia aliongoza waombolezaji kuuaga mwili wa Ndugai katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma jana.
Mwili wa kiongozi hiyo ulifikishwa katika viwanja hivyo ukiwa kwenye jeneza lililofunikwa kwa Bendera ya Taifa na ulipokelewa na Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na waombolezaji weingine.
Tangu saa moja asubuhi, mamia ya waombolezaji wakiwemo watumishi wa Bunge, watumishi wa serikali na viongozi wa vyama vya siasa walifika katika viwanja hivyo.
Kuanzia jana mchana Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi aliongoza mamia ya wananchi kuuaga mwili wa Ndugai katika viwanja vya Kongwa.
Mamia ya waombolezaji hasa wanawake walishindwa kujizuia walipouona mwili wa marehemu na kuangua vilio na kuwalazimu walinzi kufanya kazi ya ziada kuwatuliza.
Katibu wa Bunge, Baraka Leonard alisema Ndugai alizaliwa Januari 21, 1963 katika Kijiji cha Laikala, Kata ya Sagara, Wilaya ya Kongwa, Dodoma.
Alisema kiongozi huyo alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Mahambe iliyopo Ikungi, Singida kuanzia mwaka 1971 hadi 1977 na mwaka 1978 hadi 1981, aliendelea na masomo ya katika Shule ya Sekondari ya Kibaha na mwaka 1982 hadi 1984 aliendelea na elimu ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari ya Old Moshi mkoani Kilimanjaro.
“Mwaka 1988 alijiunga na Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka na kutunukiwa Stashahda ya Usimamizi wa Wanyamapori, mwaka 1990 hadi 1993 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kutunukiwa Shahada ya Sayansi katika Ikolojia na Zolojia ya Wanyamapori,” alieleza Leonard.
Leonard alisema Ndugai alichaguliwa kuwa Mbunge wa Kongwa mwaka 2000 na ameendelea kuwa Mbunge wa jimbo hilo hadi Agosti 3, mwaka huu.
Alisema kwa mujibu wa taarifa za kitabibu, Ndugai alifariki dunia Agosti 6, mwaka huu jijini Dodoma kutokana na shinikizo la damu kushuka iliyosababishwa na maambukizi makali ya mfumo wa hewa.
Leonard alisema kiongozi huyo ameacha mke, watoto na wajukuu.
Awali, Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anna Makinda alisema Ndugai alikuwa mtu mwenye akili na mbunifu jambo lililosaidia wafanye mambo mengi.
Makinda alisema tangu Ndugai alipoingia bungeni mwaka 2000 alifanya naye kazi tangu akiwa mbunge hadi alipofikia nafasi ya kuwa Spika wa Bunge.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira alisema mchango wa Ndugai ni mkubwa katika historia ya Bunge la Tanzania.
Mtoto wa Ndugai, Yustino Ndugai alishukuru wote waliojumuika nao kuomboleza na akuishukuru serikali na viongozi kwa kuwafariji.
Mwili wa Ndugai unatarajiwa kuzikwa leo kijijini kwao Sejeli, Kongwa mkoani Dodoma.