Mamlaka Ngorongoro yadhibiti ujangili

MAMLAKA ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imedhibiti ujangili wa wanyamapori hasa tembo, ndani na nje ya Hifadhi ya Ngorongoro na Pori la Akiba la Pololeti.

Kamishna wa Uhifadhi NCAA, Dk Elirehema Dorie alisema hayo Dodoma jana akieleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika eneo la utalii na uhifadhi ndani ya miaka minne tangu 2021 mpaka sasa.

Dk Dorie alisema matukio ya ujangili wa tembo yamepungua kutoka 25 mwaka 2020/2021 hadi tukio moja 2022/2023 na hakuna tukio mwaka jana.

“Matukio ya ujangili wa tembo yamepungua kutoka 25 mwaka 2020 hadi sifuri mwaka 2024 katika Ngorongoro na Pololeti. Kwa kushirikiana na vikosi vya usalama, NCAA imefanikiwa kukamata watuhumiwa 207 wa ujangili, huku mitandao ya ujangili kwa sumu na silaha za jadi ikidhibitiwa,” alisema.

Dk Dorie aliwaeleza waandishi wa habari kuwa watuhumiwa wa ujangili 207 walikamatwa na 175 wamefikishwa mahakamani.

Alisema NCAA imeangamiza mitandao ya ujangili inayotumia sumu na silaha za jadi katika maeneo mbalimbali ambapo mafanikio haya yanatokana na ushirikiano madhubuti na matumizi ya teknolojia za kisasa katika kulinda wanyamapori.

Dk Dorie alisema matukio ya uhalifu dhidi ya wageni ndani ya hifadhi yamepungua kutoka matukio saba 2020/2021 hadi sifuri mwaka jana jambo linaloimarisha usalama wa watalii.

Aidha, alisema NCAA imedhibiti migogoro ya ardhi na uvamizi wa maeneo ya hifadhi kwa kujenga vigingi 110 katika mipaka ya hifadhi kwa lengo la kuimarisha utambuzi wa maeneo yaliyohifadhiwa pamoja na kuotesha na kugawa miche ya miti 1,150,188 katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Dk Dorie alisema idadi ya wanyamapori imeongezeka na kwamba faru weusi wameongezeka kwa asilimia 40 kutoka mwaka 2020 hadi 2024.

Alisema simba wameongezeka ndani ya hifadhi na kufikia takribani 188. Tembo wameongezeka kutoka 800 mwaka 2020 hadi makadirio ya 1,300 mwaka 2024.

Dk Dorie alisema NCAA imeimarisha ulinzi wa rasilimali hali iliyosaidia kudhibiti ujangili na kurejesha mfumo wa kiikolojia wa Serengeti-Masai Mara ambao hatua hizi zimechochea urejeo wa uoto wa asili na malisho ya wanyamapori.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button